BADO hali ni tete kufuatia mwanamke mmoja, Zuhura Sudi (26), mkazi wa Mtaa wa Utusi Kata ya Chemchemi Manispaa ya Tabora kudaiwa kuwaua kwa kuwakaba shingo watoto wake wawili, Mwamvua (6) na Sudi Mrisho (miezi saba) kisha kuwazika kwenye mashimo mawili ndani ya nyumba.
Mwanamke (Zuhura Sudi) anayetuhumiwa kuwaua watoto wake.
Tukio hilo ambalo limeishangaza nchi hasa kufanywa na mama mzazi
ambaye anaujua uchungu wa kuzaa, lilijiri Jumapili usiku ndani ndani ya
nyumba ya mwanamke huyo.SIKU MOJA KABLA
Taarifa kutoka vyanzo vya uhakika, siku moja kabla ya tukio, mwanamke huyo ambaye ni mtata kiasili alionekana akicheza na watoto wake na watoto wa jirani huku akionesha uchangamfu mkubwa.
“Kama wale watoto wake wangejua mama yao mzazi ndiyo safari ya kifo chao naamini wasingemchangamkia mama yao.
“Walicheza kwa amani, kwa upendo. Kumbe mama ana mahesabu yake. Haiwezekani leo niambiwe kuwa mawazo ya kuwaua watoto wake aliyapata ghafla,” alisema shuhuda mmoja.
USIKU, JIRANI ASIKIA KISHINDO
Jirani mmoja na nyumba ilipotokea tukio alisema:
“Mimi awali ya siku ya kuelekea usiku wa tukio, nilimwona yule mama. Nikasalimiana naye. Alionekana yupo kawaida tu.
“Lakini usiku, kukiwa kumetulia nilisikia vishindo kama mtu anachimba ardhi. Nilipofuatilia nikabaini vilikuwa vikitoka upande wa nyumbani kwa mwanamke yule.“Sikushtuka. Nilijua ni shughuli zake za kawaida zinaendelea ndani ya nyumba yake. Kulipokucha sasa, nikasikia yule mama anasema kwamba watoto wake wamepotea.
“Palepale nikaanza kuhisi kitu kwa ile mishindo ya usiku. Inaonekana alishawaua watoto wake sasa alikuwa anachimba mashimo ya kuwafukia. Kule si kuwazika na yale si makaburi ni mashimo.
“Inauma sana, siamini kama mama aliyezaa watoto kwa uchungu mkubwa anaweza kufanya ukatili kama huu.”
Miili ya watoto hao baada ya kufukuliwa kwenye mashimo.
AKILI ILIMWAMBIA ASUBIRI AKIWA PEKE YAKEBaadhi ya majirani walisema ndani ya nyumba hiyo kuna watu wengine wanaishi, lakini mtuhumiwa huyo alisubiri akiwa peke yake ndipo akatekeleza ukatili wake wa kutisha.
ANACHOJUA MWENYEKITI WA MTAA
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Utusi, Aziza Mwenya, ushirikiano mkubwa kati ya wananchi wa mtaa huo ndiyo uliofanikisha kugundulika kwa tukio hilo la kinyama lililopoteza maisha ya watoto hao wasiokuwa na hatia.
“Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa babu wa Zuhura, mzee Shaban Ramadhan kuhusu kutoweka kwa watoto hao katika mazingira ya kutatanisha, tulifika kwenye nyumba ya tukio kwanza na kumhoji mama wa watoto.
Ndugu na majirani wakiwa na makamanda wa Polisi eneo la tukio.
“Cha ajabu alikuwa akizuia watu kuingia ndani. Kumbe alishajua
kinachoendelea na akiruhusu sisi kuingia nini kitatokea.“Hata hivyo
majirani kwa kushirikiana na mimi na baba wa mmoja wa watoto waliouawa
(Sudi Mrisho), Mrisho Abdallah tulimshika kwa nguvu Zuhura, watu
wakaingia.”WAKUTA MASHIMO MAWILI
“Tulipofika, tukabaini mashimo mawili aliyokuwa amewafukia watoto wake. Shimo moja sebuleni, jingine chumbani. Tuliwapa taarifa polisi wakafika haraka sana. Mashimo yalipofukuliwa, watoto walikutwa ndani ya mifuko miwli ya sandarusi. Inauma sana. ”
MTUHUMIWA AZUNGUMZA NA AMANI
Amani lilibahatika kuzungumza na mwanamke huyo katika mahojiano mafupi akiwa chumbani muda mfupi kabla ya polisi kufika.Amani: “Hivi Zuhura, ni kwanini umeamua kuwaua watoto wako wa kuwazaa?”
Zuhura: “Nani? Mimi sijui, we (mwandishi) ndiyo unajua.”Amani: “Watoto wako wako wapi?”
Zuhura: “Nani? Wako wapi kwani?”
KILICHOONEKANA
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo walisema, Zuhura licha ya kuonekana hana wasiwasi wowote, lakini pia aliashiria kujitoa ufahamu ili atafsirike kwamba hakuwa na akili timamu.
KUMBUKUMBU MBAYA
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa majirani zinadai kuwa, mwaka 2013, Zuhura alidaiwa kumsababishia kifo mtoto wake mchanga wa kiume kufuatia kumzidishia dozi ya malaria wakati alipokuwa akiumwa.
KAMANDA WA POLISI
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Juma Bwire ilikiri kutokea kwa tukio hilo.
Afande Bwire alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
No comments:
Post a Comment