SIKU chache baada ya Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Uzima na Ufufuo la jijini Dar, Josephat Gwajima kumtusi Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini, Polycarp Kardinali Pengo, taarifa nyuma ya pazia zimeeleza kuwa mchungaji huyo ametumwa na kikundi cha watu fulani, Uwazi Mizengwe linakupa mchapo kamili.
Gwajima alirekodiwa kwenye ibada ya kanisa lake Jumapili iliyopita ambapo ‘alimtusi’ Pengo akituhumu kuwa ni msaliti kwani amekwenda kinyume na Taasisi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa kuwataka waumini waisome Katiba Inayopendekezwa kisha wapewe uhuru wa kupiga kura ya “ndiyo” au “hapana” tofauti na vyombo hivyo vyenye dhamana ya kuongoza dini ya Kikristo vilivyotaka waumini waipigie kura ya “hapana” Katiba Inayopendekezwa.Kwa mujibu wa chanzo chetu, Gwajima ametumwa na kikundi cha watu ambacho kinaunga mkono hoja ya kukataa Mahakama ya Kadhi kama ilivyokataliwa na vyombo hivyo vyenye dhamana ya kuongoza dini ya Kikristo hivyo kumpinga Pengo ambaye wanaamini anatetea suala la Mahakama ya Kadhi liruhusiwe.
“Gwajima anatumika tu anamkashifu Pengo ili kumchafua na asiweze kusimamia hoja yake ya kuwaacha wapigakura waamue wenyewe kuikubali au kuikataa Katiba Inayopendekezwa wakiamini watu wanaweza kuipigia kura ya “ndiyo” na suala hilo likajadiliwa wakati wenzake wamelipinga,” kilisema chanzo hicho.
Kama hiyo haitoshi, chanzo hicho kilizidi kudai kuwa, Gwajima ametumika kumchafua Pengo kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kuhofia huenda akawa na upande wa mgombea ambaye anampigia chapuo ili apitishwe.
“Siyo tu kuhofia Mahakama ya Kadhi, Gwajima ametumika kumchafua Pengo kwa hofu kuwa huwenda akawa ana mgombea wake anayemtaka awe rais,” kilisema chanzo hicho.
Jitihada za kumpata Gwajima ili aweze kuzungumzia madai hayo hazikuzaa matunda kufuatia simu yake kutopatikana hewani lakini gazeti hili liliweza kuzungumza na mmoja wa viongozi wa chini yake aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini ambapo alisema Gwajima anatumika na Roho Mtakatifu na si vinginevyo.
“Mchungaji (Gwajima) ametumwa na Roho Mtakatifu kusema yale aliyoyasema hakutumwa na mtu wala kikundi chochote cha wanasiasa,” alisema kiongozi huyo.
No comments:
Post a Comment