Muigizaji Vincent Kigosi ‘Ray’.
INGAWA bado anaonekana kijana mdogo kiumri, tofauti
na unavyoweza kumchukulia mtu kama Amri Athuman ‘King Majuto’, lakini
katika uigizaji wa filamu, Vicent Kigosi maarufu kama Ray, ni mmoja wa
wacheza filamu wakongwe hapa nchini.Hii ni kwa sababu wao ndiyo vijana wa mwanzo mwanzo kujiingiza katika sinema za kizazi kipya, pale filamu ya Girl Friend ilipofungua pazia mwanzoni mwa miaka ya 2000, kwani kabla ya hapo, tulizoea michezo ya maigizo katika runinga na redio, heshima kwao King Majuto, Mzee Small, Bi Chau, Mzee Jangala na wenzao.
Ninamfahamu kidogo Ray, tangu wakati ule akiwa na Kaole na wenzake wakifanya tamthiliya zilizorushwa na Kituo cha ITV. Hii siyo mara yangu ya kwanza kumzungumzia hapa, kwa maana hiyo, sina maneno mengi yanayoongelea kuhusu yeye ana umahiri gani hasa kwa sababu mashabiki wa tasnia ya filamu watakuwa wanamfahamu vyema.
Ni vigumu kumkuta shabiki wa filamu za Kibongo akiwa hana CD ya Ray, ingawa pia wanaweza kuwa wapo ambao hawathamini mchango wake katika game. Kwa sisi tunaofahamu kidogo, ni jambo lisilowezekana kuizungumzia tasnia hii bila kuliweka mbele jina la Vicent Kigosi.
Ingawa ana jina kubwa katika uigizaji, linalomfanya kuwa miongoni mwa mastaa wanaotazamwa zaidi Bongo, bado nje ya fani yeye ni kijana wa kawaida kabisa, akitoa ushirikiano mzuri anapohitajika na ni mwepesi kuchangia mada katika mazungumzo yoyote yanayomshirikisha. Ingawa wapo wanaodai mshkaji ana nyodo, kwangu mimi sitaki dhambi, sijawahi ona nyodo zake!
Juzikati, Ray alikuwa mmoja wa mashabiki waliojitokeza kwa wingi katika shoo ya Christian Bella pale Escape One, jijini Dar ambako watu wa muziki wa kizazi kipya walipata burudani nzuri kutoka kwa wasanii mbalimbali kama Ali Kiba, Kassim Mganga na mwanadada Alicios Theluji.
Ray alikuwa katika meza moja na washkaji zake, wakiwemo waigizaji wenzake, wakipata kinywaji taratibu huku stori zikiendelea. Lakini katika jambo lisilotarajiwa, wakati mmoja staa huyo alipoinuka, kutokana na ufupi wa shati lake, silaha aina ya bastola ilionekana ikiwa imechomekwa kiunoni mwake upande wa mgongo.
Sifahamu kuhusu mamlaka ya Escape One inasema nini juu ya watu kuingia na silaha ukumbini, lakini shida yangu hasa ipo kwa Ray, kwa sababu nina uhakika wa 100%, silaha ile ilikuwa ni kwa ajili ya ulinzi wake binafsi.
Ulinzi binafsi una maana pana. Maana ya msingi kabisa ni kutambua na kuelewa maeneo na mazingira hatari kwa mmiliki wa silaha, hasa anayetumia kiburudisho, kama ilivyo kwa rafiki yangu Ray.
Nadhani busara inamzuia mwenye silaha ya kujilinda kukaa sehemu yenye uwezekano mkubwa wa kutokea kwa matukio ya kulazimisha matumizi ya silaha.
Katika starehe kama ile kwa mfano, kijana mmoja aliyejilewea zake, anaweza tu kuamua kumvaa staa yeyote kwa kuamini kuwa anajidai au kujisikia. Akamfanyia fujo. Tunajua, mara nyingi baada ya kiburudisho kuanza kufika levo zake, watu huwa hawajali na tena hutamani sana kuwasemea ovyo mastaa.
Ikitokea hivyo, kwa jinsi mastaa wetu walivyo, nao huwa hawakubali, ni wepesi wa kushambulia. Je, ukiwa na ‘mkwaju’ kiunoni, si ni rahisi kupiga, hasa kama mtu atakwambia bastola hiyo toi haina lolote huku anakufuata?
Kuna mengi ya kufikiri, huenda ni kweli ni silaha kwa ulinzi wake au pengine, alifanya hivyo ili kuwaonyesha watu kuwa anamiliki bastola. Kama hili la pili ndilo linalohusika, nimtahadharishe kuwa makini, maana anaweza kujutia uamuzi wake wa kwenda kwenye starehe akiwa na ‘cha moto.’
Na mwisho, nimshauri kubeba silaha katika eneo lile tu analoamini chochote kinaweza kutokea. Kuna maeneo unaweza kwenda na kumudu kujilinda kwa kuchunga kauli tu!
No comments:
Post a Comment