Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli.
Na Ibrahim Mussa, Dar es SalaamHAKUNA kauli nyingine ambayo unaweza kuitumia kwa sasa badala ya kusema kuwa Yanga haizuiliki kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara, baada ya jana kuichapa Mbeya City kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga iliingia uwanjani ikiwa na rekodi ya pekee baada ya wiki moja nyuma kushinda kwa mabao 8-0 dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja huo.Matokeo hayo yanaifanya Yanga ishinde mechi tano mfululizo za ligi, ikiwa na maana kwamba tangu ifungwe na Simba Machi 8, mwaka huu imegeuka mbogo na kuanza kutoa vipigo.
Waliokumbwa na vipigo vya Yanga baada ya Machi 8 ni Kagera, Mgambo, JKT Ruvu, Coastal Union na Mbeya City. Lakini Yanga pia imeweka rekodi ya kufunga mabao 18 ndani ya mechi tano zilizopita huku Simon Msuva akitupia matano na Amissi Tambwe akifunga sita katika mechi hizo.
Hii inamaana kuwa hivi sasa Yanga haizuiliki na kila atakayekatiza mbele yake inamtembezea kipigo tu.
“Ukweli tulikuja uwanjani tukihitaji ushindi, lakini hatuna jinsi tulizidiwa na Yanga wakatumia nafasi hiyo kupata ushindi, hakika sasa tunakwenda kujiandaa na mchezo wetu ujao dhidi ya Simba,” alisema kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi.
Katika mchezo wa jana, Yanga walionyesha kiwango cha hali ya juu kuanzia mwanzoni mwa mchezo huo hadi mwisho, hali iliyowafanya mashabiki wao kushangilia kwa muda wote.Ushindi huu unamaanisha kuwa tangu Mbeya City wapande daraja hawajawahi kuibuka na ushindi hata mara moja kila wanapokutana na Yanga wakiwa wamefungwa mara tatu na kutoka sare mara moja.Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Yanga walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Yanga walianza kuongoza katika dakika ya 18 tu, baada ya mshambuliaji wake raia wa Liberia Kpah Sherman kuifungia timu hiyo bao safi baada ya kumzidi ujanja beki wa City, Juma Nyosso.Hili ni bao la pili kwa mchezaji huyo msimu huu akiwa amefunga bao la kwanza kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union wiki iliyopita na sasa anaonekana kuanza kazi.
Bao la pili liliwekwa kimiani na kiungo mstaarabu Salum Telela, katika dakika ya 37, akipiga shuti kali ambalo lilimpoteza kipa wa City. Alipata pasi safi kutoka kwa Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.Hili ni bao la pili kwa Telela msimu huu, ukiwa ndiyo msimu alioonyesha kiwango cha juu sana tangu ameanza kucheza soka.
Dakika mbili baadaye, Mbeya City walijipatia bao moja, shukrani kwa bao safi lilofungwa na Themi Felix ambaye aliwazidi ujanja mabeki wa Yanga.Kipindi cha pili hakikuwa kizuri kwa vijana wa Mbeya ambao msimu uliopita walimaliza wakiwa nafasi ya tatu baada ya dakika nne tu Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuifungia timu yake bao la tatu kwa kichwa, likiwa ni la pili kwake kwenye Ligi Kuu msimu huu.
Hii ina maana kwamba wachezaji wote waliofunga mabao ya Yanga jana walikuwa na bao moja moja na hayo ni mabao yao ya pili.Dakika ya 53 Mbeya City walipata pigo lingine baada ya Felix kupewa kadi nyekundu kutokana na kumchezea rafu Telela.
Hata hivyo, rafu hiyo ilikuwa mbaya kwa mchezaji huyo tegemeo kwa Yanga msimu huu baada ya kushindwa kurejea uwanja na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Dilunga.Yanga pia walimtoa Sherman na kumuingiza Mrisho Ngassa.
“Tumepata ushindi kwa kuwa tulitumia vyema nafasi tulizopata mwanzoni, mabao ya haraka yalitusaidia kulinda ushindi wetu, najua kuwa tuna mchezo mgumu wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Etoile, hakika tunajiandaa vyema kukabiliana nao,” alisema Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm.Katika mchezo mwingine, Stand wameichapa Polisi Morogoro kwa bao 1-0.
No comments:
Post a Comment