Mshambuliaji wa Free State Stars ya Afrika Kusini, Mrisho Ngassa.
Sweetbert Lukonge, Dar es SalaamUNAWEZA kusema kitumbua kimeingia mchanga! Uamuzi wa kumzuia mshambuliaji Mrisho Ngassa kuitumikia klabu yake mpya ya Free State Stars ya Afrika Kusini, utapitishwa ndani ya siku chache.
Taarifa za uhakika zinaeleza, Ngassa hataruhusiwa kucheza nchini Afrika Kusini alikojiunga na klabu hiyo kwa miaka minne kwa kuwa klabu yake ya zamani ya Yanga imeandika barua kutaka uhamisho wake wa kimataifa (ITC) uzuiwe hadi atakapolipa deni linalokadiriwa kufikia Sh milioni 40.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Benki ya CRDB zimeeleza Ngassa aliyekopa Sh milioni 45, aliacha kulipa fedha hizo kwa muda mrefu hadi alipoanza kufanya hivyo miezi michache iliyopita.“Kweli hakuwa akipeleka fedha kwenye akaunti yake, hata mshahara haukuwa ukienda na tulipofuatilia tulielezwa kwamba alikuwa akichukulia dirishani, tuliwasiliana na uongozi wa Yanga, mshahara wake ukaanza kuwekwa kwenye akaunti.
“Sasa tumesikia anakwenda Sauz kucheza huko, tumeuliza kuhusu deni letu, ikaonekana Yanga wanataka tuwasiliane naye. Imeonekana ni vigumu kumpata Ngassa, hivyo tumeandika barua ITC izuiwe.“Tumewasisitiza hilo Yanga kwa kuwa ndiyo walimuwekea dhamana. Tunaamini itazuiwa kwa kuwa hata TFF wanajua maana ya utaratibu wa madeni, hivyo tunawaachia kwa muda,” kilieleza chanzo muhimu.
Kwa upande wa Yanga, Mkuu wa Kitendo cha Mawasiliano, Jerry Muro, alisema: “Sijapata hizo taarifa kutoka kwa uongozi, zikifikia basi nitawataarifu.”Gazeti hili liliamua kuwatafuta TFF na msemaji wake, Baraka Kizuguto alisema pia hakuwa na taarifa hizo.
“Hizi kwangu ni mpya, lakini hadi sasa hakuna maombi ya ITC ya Ngassa. Labda barua haijafika, tusubiri ikifika itawasilishwa kwa uongozi na wenyewe utajua cha kufanya ni kipi.”Ingawa juhudi za kumpata Ngassa zilikuwa tatizo kubwa kutokana na simu zake zote kuwa zimezimwa, hata Championi Ijumaa lilipopiga hodi nyumbani kwake bado ikaelezwa hakuwepo, lakini taarifa za ndani za Yanga zinasema wanatambua alilipwa Sh milioni 90.
“Tulisikia ikielezwa Ngassa amelipwa dola laki moja na hamsini (zaidi ya Sh milioni 300), sisi tunajua amepokea Sh milioni 90. Lingekuwa jambo zuri sana kama angemalizana na CRDB, ili aende kwa amani.
“Kweli kuna mpango huo, lakini uongozi ndiyo utashughulikia. Hauwezi kumuacha Ngassa aende na deni halafu klabu isumbuke, nafikiri wasilianeni tena na uongozi unaweza kuwapa ufafanuzi,” kilieleza chanzo cha karibu kabisa na uongozi wa Yanga.
Fedha hizo ni mkopo aliochukua Ngassa ili kuilipa Simba baada ya TFF kumuamuru afanye hivyo kufuatia kubainika alikuwa akidaiwa na Simba baada ya kuchukua Sh milioni 30, huku Sh milioni 15 zikiwa ni kama adhabu.
Kutokana na hali hiyo, TFF ilimfungia Ngassa kucheza mechi sita za Ligi Kuu Bara, pia kulipa faini hiyo ambayo alilazimika kukopa CRDB huku Yanga ikimuwekea dhamana.
No comments:
Post a Comment