Baada ya vuta vikuvute ya muda mrefu, hatimaye leo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kumtangaza mgombea wake wa urais katika mkutano maalumu utakaofanyika jijini Mwanza.
Habari
zilizopatikana na kuthibitishwa na viongozi wa chama hicho Kanda ya
Ziwa Magharibi na makao makuu zilisema kuwa leo mgombea huyo atatangazwa
mkoani hapa huku zikibainisha kuwa anayepewa nafasi kubwa ni Katibu
Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa.
Taarifa
hizo zimekuja wakati kukiwa na tetesi kuwa chama hicho kilikuwa
kinafanya mazungumzo na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyekuwa
anawania urais kupitia CCM na kutemwa katika hatua za awali, huku vyanzo
mbalimbali vikisema mazungumzo hayo yanachukua muda mrefu na kuna
uwezekano mkubwa wa kutozaa matunda.
Jana,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na baadhi ya wabunge
walikaririwa wakitoa matamko ya kumkaribisha Lowassa kuingia Chadema
lakini kwa sharti la kufuata kanuni na taratibu za chama hicho, lakini
Dk Slaa alisita kumzungumzia kiongozi huyo akiahidi kuzungumza mambo
yatakapokuwa sawa.
Mratibu
wa Operesheni za Chadema Kanda ya Ziwa Magharibi, Tungaraza Njugu
alisema mgombea huyo (bila kumtaja jina), atatangazwa katika mkutano wa
hadhara utakaofanyika kwenye Viwanja vya Magomeni, Ilemela kuanzia saa
nane mchana.
Njugu alisema katika mkutano huo, viongozi wakuu wa Ukawa wanatarajia kuwapo na maandalizi yake yamekamilika.
“Kesho (leo) tutakuwa na mkutano mkubwa kwenye viwanja vya Magomeni,” alisema Njugu na kuongeza: “Mgombea urais kupitia Ukawa atajulikana hapo, kwani tunatarajia viongozi wakuu wa Ukawa watamtangaza.”
Katika
mazingira tofauti, akihutubia mkutano wa hadhara mjini Geita juzi,
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alidokeza jina la Dk Slaa kama
mgombea urais wa chama hicho, kitendo kilichoibua hamasa na umati
kumshangilia, lakini akawapoza akisema ulimi umeteleza.
Alipoulizwa
kuhusu mkutano huo, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikiri kuwa
leo kulikuwa na mpango wa kumtangaza mgombea wa Ukawa, lakini alidhani
ingekuwa Dar es Salaam, hivyo kwa kuwa wameamua iwe Mwanza angefanya
utaratibu wa ndege ili aweze kuwahi.
Mwenyekiti
wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia hakupatikana kuzungumzia mkutano huo,
lakini Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe alisema hakuwa na
taarifa hizo, hasa kwa kuwa vikao vya mwisho vilivyofanyika Jumapili na
Jumatatu vilihusisha wenyeviti wa vyama pekee.
Hata
hivyo, alisema ilibidi mgombea huyo atangazwe ama jana au leo. Chama
cha CUF kimekwishatangaza kuwa kinasubiri uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu
la Uongozi litakaloketi Julai 25 kuamua juu ya hatima yake ndani ya
Ukawa.
Alipotakiwa
kudokeza ni nani atasimama kuwakilisha Ukawa, Njugu alisema jukumu hilo
ni la viongozi wa juu na kwamba yeye akiwa kiongozi wa Kanda anatambua
mgombea urais wa Ukawa atatangaziwa Mwanza leo.
Mkutano
huo utakaorushwa moja kwa moja katika televisheni, pia unatarajia
kumpokea Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya aliyetangaza
kukihama chama hicho juzi bila kuweka wazi anakohamia.
Hata
hivyo, mbunge huyo ambaye tayari ameweka wazi kupitia ukurasa wake wa
Facebook kuwa atawania ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini, amekaririwa
akisema hatima yake itakuwa hadharani leo.
No comments:
Post a Comment