Wakati pazia la kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba likisubiri kufunguliwa kesho, Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali haitasita kufungia chombo cha habari kitakachotumia uhuru wake kuleta uchochezi na vurugu nchini.
Hiyo ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kutoa kauli kama hiyo mwaka huu. Machi wakati wa mahojiano maalumu na Naibu Mkurugenzi wa Azam TV, Tido Mhando kwenye hafla ya uzinduzi wa studio za Kituo cha Televisheni cha Azam, alionya kuwa Serikali haitavumilia vyombo vya habari endapo vitumia uhuru wao kuchochea chuki, vurugu na mifarakano nchini.
Jana, wakati akitoa hotuba yake alipotembelea Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora jijini hapa, alirudia kauli hiyo na kusema; “kama watu watatumia uhuru wa vyombo vya habari kuchochea vurugu tutawafungia… huwezi kupewa uhuru na kuamua kufanya lolote.”
“Ndiyo maana nasema kila kitu kina ukomo wake, uhuru huo (wa vyombo vya habari) hauwezi tu kuwa wa kufanya lolote. Serikali inao wajibu kwa sababu tunaheshimu sana uhuru wa habari. Lakini mkichochea mgogoro kati ya Wakristo na Waislamu, Wagogo na Warangi hili hatukubali kwa sababu mtakuwa mmekwenda nje ya uhuru tunaoutaka,” alisema.
Rais Kikwete alisema aliwahi kuhojiwa na mwandishi wa habari wa Kenya kuhusu kufungia baadhi ya magazeti nchini kuwa ni kukiuka uhuru wa vyombo vya habari, naye akamjibu kwa swali kuhusu uchochezi wa machafuko ya nchi hiyo mwaka 2007.
“Nilimwambia mbona wasiiambie hivyo Mahakama ya ICC… kuna mwandishi wa Kenya ambaye chombo chake kilihusika na uchochezi kwenye uchaguzi na sasa ana kesi... kumjibu vile, yule mwandishi hakuuliza tena,” alisema.
Alitoa mfano wa machafuko yaliyowahi kutokea Rwanda kwamba yalichochewa na vyombo vya habari hadi kufikia hatua ya wananchi wengine kuitwa mende.
Alisema upo uhuru wa kuikosoa Serikali na kwamba ikisemwa inajiweka sawasawa, huku akisisitiza kuwa nchi haijamshinda kama baadhi ya watu wanavyosema.
“Katika kipindi hiki nimejitahidi kuwaachia, watu wako huru, wengine wanamwaga mpaka radhi kama wapo kwenye mdundiko,” alisema.
Kuhusu migogoro ya ardhi, alisema baadhi inasababishwa na watumishi wasiofuata sheria hasa mijini na wananchi kutokufahamu haki zao kuhusu matumizi ya ardhi.
Aliitaka tume hiyo iendelee kutoa elimu ili wananchi wafahamu haki zao.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Tom Nyanduga alimwomba Rais Kikwete kushughulikia suala la bajeti ndogo kwa tume hiyo akisema linakwamisha utendaji wao wa kazi.
“Naamini katika siku 65 zilizobaki unaweza kuisaidia tume kwa kuendelea kuwa wakili namba moja kupigia debe suala hili,” alisema Nyanduga.
Mbali na ombi hilo, Nyanduga alimpongeza Rais Kikwete ambaye anakaribia kumaliza kipindi chake cha uongozi kwa kuiacha nchi ikiwa salama.
“Tume inakupongeza kwa kudumisha utulivu na amani, umesimamia pia haki na misingi ya utawala bora kwa kipindi ulichokuwa madarakani,” alisema.
Alisema katika kipindi chake, Rais Kikwete amesimamia mabadiliko na kuwezesha mhimili wa Mahakama ambayo ni nguzo kuu ya kulinda haki za binadamu, kutekeleza majukumu yake kwa kikamilifu.
Kuhusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), alimpongeza kwa juhudi alizofanya katika kukemea mauaji hasa kwa kuhamasisha tume hiyo na wadau kuandaa mpango kazi wa kuyapinga.
“Mauaji hayo yalianza kutia doa nchi yetu hasa kwa mataifa ya nje, lakini kauli yako ya kukemea mauaji na ukatili huo, imeonyesha dhahiri kuwa hukupendezwa nayo,” alisema.
No comments:
Post a Comment