MAYASA MARIWATA NA BONIPHACE NGUMIJE
MWANAMITINDO Jokate Mwegelo ‘Kidoti’ na mwandani wake Ally Salehe Kiba, wamethibitisha kuwa wana maelewano mazuri (picha zinaiva) baada ya mwishoni mwa wiki kuonekana pamoja katika bonanza maalum la wanafunzi, lililofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lililojulikana kama Kidoti Bonanza liliandaliwa maalum kwa ajili ya kuthamini vipaji vya wanafunzi na ambalo lilihudhuriwa na madenti wa shule mbalimbali ambao pia walipata burudani kutoka kwa wasanii na makundi tofauti.
Jokate alikuwa jukwaani pamoja na msanii anayetamba na kibao cha Ni Yule, Hellen George ‘Ruby’ ambaye alishika kipaza sauti na kuwauliza madenti hao kama wanafahamu mtu aliyeimbwa na Kidoti katika kibao chake cha Leoleo ambao wote kwa pamoja walijibu kuwa mtu huyo ni Ali Kiba.
….Wakiwa stejini.
“Hivi nataka niwaulize, mnajua ile nyimbo Jokate aliposema anamvizia anapokatisha akienda mpirani alikuwa kamlenga nani,” aliuliza Ruby ambaye alikuwa ‘akimkata’ jicho Jokate aliyekuwa akiangua kicheko muda wote.
Muda mchache baadaye, Ally Kiba aliwasili eneo hilo akiwa ameongozana na dada yake Zabibu na alipokaribia jukwaani, Jokate alimkimbilia na kumkaribisha kwa busu na baadaye kukumbatiana bila kujali macho kodo ya madenti.
Kama hiyo haitoshi, mkali huyo wa Bongo Fleva alipopanda jukwaani kutumbuiza kwa sapraizi, watu walimgomea na kutaka ampandishe Jokate acheze naye na kujikuta akifanya hivyo, japo mwanadada huyo alionekana kuona aibu kucheza na mwandani wake huyo, wakabaki kuangaliana jambo lililozua shangwe na kuwalazimu kucheza Wimbo wa Chekecha-Cheketua baada ya Kiba kumlazimisha mlimbwende huyo acheze.
Jokate alipoulizwa na paparazi wetu aliishia kucheka na kuomba aachwe kwa muda huo kwa kuwa alikuwa `bize’, lakini ‘King Kiba’ alisema uwepo wake eneo hilo ni jambo linalojionyesha wazi kwani hakuna siri tena.
“Sipendi kuyaongelea hayo mambo, lakini hiyo imeshakuwa gumzo la jiji na nyinyi kama wanahabari kila kitu kinajionesha, kama kusoma huwezi basi hata picha huoni? Kilichonileta hapa ni kumsapoti Jokate sababu kitu anachokifanya ni kizuri na nitamuunga mkono mwanzo mwisho katika kila jambo.”
CHANZO: GPL
No comments:
Post a Comment