MABINGWA wa Soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga ya jijini Dar
es Salaam, wametangaza kuwatema wachezaji wake 11 kwa ajili ya Ligi Kuu
Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mchakato
wa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara kuwasilisha majina ya wachezaji
wanaoachwa ama kumaliza mikataba unafikia tamati kesho.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema jijini Dar es Salaam jana
kwamba klabu yake imewaacha wachezaji hao, ambapo kati yao kuna
waliomaliza mikataba yao na wengine kupelekwa kwa mkopo klabu nyingine
za Ligi Kuu bara.
Aliwataja wachezaji walioachwa kuwa ni pamoja washambuliaji wa
kimataifa, Mghana Keneth Asamoah na Mzambia Davies Mwape, huku wengine
wakiwa Iddi Mbaga, Julius Mrope, Kiggi Makassi, Atif Amour, Abuu Ubwa,
Zuberi Ubwa, Bakari Mbegu, Godfrey Bonny na Shaban Kado ambaye
amepelekwa kwa mkopo Mtibwa Sugar.
Aidha Sendeu alisema kikosi cha Yanga kinaendelea na maandalizi yake,
ambapo kesho kitashuka katika dimba la taifa jijini Dar es Salaam
kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki na mabingwa wa soka nchini
Uganda, Express.
Alisema, Express ilitarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam jana,
ambapo kiingilio kitakuwa ni sh 20,000 kwa VIP A, sh 15,000 VIP B na C,
sh 5,000 kwa watakaokaa viti vya kijani na wale watakaokaa viti vya
rangi ya bluu na chungwa watalipa sh 3,000.
Katika hatua nyingine, klabu hiyo leo inatarajiwa kuendesha kisomo
maalum ‘hitma’ kwa ajili ya kuwarehemu wanachama, mashabiki, wapenzi na
wachezaji wa timu hiyo waliotangulia mbele ya haki, ambapo zoezi hilo
litafanyika makao makuu ya klabu hiyo yaliyoko mitaa ya Jangwani na
Twiga na kuongozwa na Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali.
“Kama mnavyojua, kila msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara
unapokaribia kuanza, huwa tunasoma dua ya kuwarehemu wadau mbalimbali wa
Yanga waliotangulia mbele ya haki, hivyo kesho (leo), majira ya saa
sita mchana, hapa klabu tutaendesha kisomo hicho ambacho kitaongozwa na
Sheikh Akilimali (Ibrahim), hivyo tunaomba Wanayanga kujitokeza kwa
wingi,” alisema Sendeu.
Sendeu aliongeza kuwa baada ya dua hiyo, jioni ya leo kutakuwa na
mkutano maalumu utakaohusisha wenyeviti na makatibu wa matawi yote ya
Yanga ya jiji la Dar es Salaam.
Chanzo cha habari na Dina Ismail wa Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment