HOFU ya kutekwa, kuteswa na kupelekwa katika msitu wa Mabwepande
kama ilivyokuwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk.
Stephen Ulimboka, imeanza kumtesa Rais wa Chama cha Walimu (CWT),
Gratian Mukoba.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Mukoba alisema amekuwa akipata
vitisho vya kumzuia kushiriki kwenye mgomo walioupanga kuuanza kesho,
lakini amedai vitisho hivyo havimzuii kuendelea na mkakati wa kutafuta
haki za walimu.
Mukoba alisema hata kama atapelekwa katika msitu huo uliojipatia
umaarufu mkubwa kwa kutumiwa kuendesha vitendo vya utesaji na uuaji,
bado ukweli utabaki palepale kuwa walimu wana madai ya msingi ambayo
yamekuwa yakipigwa danadana na serikali.
Alibainisha kuwa watu wanaofikiri kuwa paka anaweza kugeuka simba
wanajidanganya kwa sababu haki ya mtu haiwezi kuminywa na mtu yeyote
hata kama ana madaraka makubwa.
“Unapomuona paka nyumbani kwako huwezi kumwita simba …eeh hata kama
napata vitisho havitanifanya kuacha kutimiza majukumu yangu, hata kama
mimi nitapata matatizo wapo watakaoendelea na kupigania haki za walimu,
kwakuwa huwezi kuzuia na kumnyamazisha kila mtu, hasa katika masilahi ya
taifa,” alisema.
Alisema anaamini kuwa kile kilichomtokea Dk. Ulimboka hakitaweza
kumtokea yeye kwa sababu watetezi mbalimbali na mikataba mingi ya
kimataifa ipo na inasimamiwa kikamilifu na watu wasiopenda haki za watu
zipotee.
Mukoba alisema serikali haina haja ya kutoa vitisho kwa walimu kuwa
mgomo wao ni batili bali iueleze umma ni kesi gani na namba ngapi
iliyopo mahakamani inayozuia mgomo huo.
“Serikali imezoea kupiga porojo za kisiasa, porojo zao hazituzuii wala
kutunyamazisha kuendelea na msimamo wetu wa kuanza mgomo kesho,”
alisema.
Fomu za serikali
Serikali imesambaza fomu kwa maofisa elimu wa wilaya ikiwataka
wazigawe kwa walimu na wajaze haraka ili wabaini wanaounga au kupinga
mgomo huo.
Fomu zimeandikwa maneno ya ‘Haraka Sana’, zina sehemu mbalimbali
ambazo zinamtaka mwalimu kuandika namba yake ya hundi, kuunga mkono
mgomo au kutounga mkono.
Kwa mujibu wa Mukoba, sehemu ya namba ya hundi imewekwa mahususi kuwakata mishahara walimu watakaoshiriki kwenye mgomo huo.
“Nawaomba walimu waendelee na msimamo wao, maana wasiposimama imara
kutetea haki zao hakuna atakayewasaidia, mgomo huo hautaathiri utumishi
wao, kwa kuwa umezingatia sheria,” alisema na kukiri kuwa kutakuwa na
vitisho na propaganda nyingi kutoka kwa waajiri.
Kuhusu suala la serikali lililopo mahakamani, Mukoba alisema hatua
hiyo haiondoi taratibu za mgomo na kuongeza kwamba serikali isitake
kutumia kivuli cha mahakama kukandamiza haki za walimu ambao
wamezingatia taratibu na sheria zote za nchi katika mgomo huo.
Juzi CWT kilitangaza mgomo rasmi huku kikikamilisha taratibu za mgomo
kwa kupiga kura kuunga au kukataa mgomo huo, ambapo kati ya walimu
183,000 walimu 153,848 sawa na asilimia 95 ya walimu waliunga mkono
kufanyika kwa mgomo.
Hatua hiyo imekuja baada ya serikali na CWT kushindwa kufikia makubaliano katika siku 30 walizoipa kuanzia Juni 25 mwaka huu.
Madai makubwa ya walimu katika mgomo huo, mbali na malimbikizo ya
madeni yao ya huko nyuma, pia wanataka ongezeko la mishahara kwa
asilimia 100, posho za kufundishia kwa walimu wa sayansi asilimia 55 na
walimu wa masomo ya sanaa asilimia 50 na posho za mazingira magumu
asilimia 30.
Mara baada ya tishio hilo la CWT, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ofisi ya
Rais (Ikulu), kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Peniel Lyimo,
juzi ilitoa taarifa kupinga mgomo huo kwa madai kuwa ni batili, kwa
sababu kuna kesi mahakamani inayozihusu pande hizo mbili.
“Kwa sasa shauri hili liko Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na leo hii
siku ya Ijumaa Julai 27, 2012 majira ya saa sita mchana pande zote mbili
zilifika mahakamani na mahakama ikaamuru kwamba pande zote zikamilishe
maelezo yao ifikapo siku ya Jumanne Julai 31, 2012 saa sita mchana ili
kuiwezesha mahakama kuendelea kusikiliza shauri hilo na hatimaye kutoa
uamuzi. Kwa hiyo mgomo huo si halali kwa vile shauri hilo bado liko
mahakamani,” ilisema.
Maandalizi mikoani
Mkoani Mbeya, Kaimu Katibu wa CWT Mkoa wa Mbeya, Felix Mnyanyi,
alisema mazungumzo kati ya walimu na serikali yameshindikana baada ya
kuthibitishwa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na kesho walimu
watagoma.
Mkoani Mara, Mwenyekiti wa CWT wilayani Bunda, Francis Ruhumbika,
amewataka walimu wote kushiriki kwenye mgomo huo kwa kutokwenda kwenye
vituo vyao vya kazi.
No comments:
Post a Comment