KATIBA YA NCHI SI MALI YA WANA CCM ASEMA HASSAN NASSOR MOYO MUASISI WA MAPINDUZI NA MUUNGANO WA TANZANIA, ATAKA CCM ISIHODHI MJADALA WA KATIBA.
01/08/2012
Na Abdallah Vuai
Katiba ya nchi sio mali ya Chama cha siasa, ingawaje baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar vyama vingi vya siasa vilifutwa na kutangazwa kuwepo kwa vyama viwili tu yaani ASP kwa Zanzibar na TANU kwa Tanganyika, hivyo kufanya katiba kuwa mali ya vyama hivyo.
Ilivyokuwa katiba katika Taifa lolote la kidemokrasia, lenye kuheshimu misingi ya utu ni mali ya wananchi na hivyo ni wananchi pekee ndiyo wenye haki ya kubadili katiba ya taifa lao.
Aidha, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni ya Watanzania wote na kamwe si ya chama tawala cha CCM, makada wake au makamanda wa vita vya ufisadi, hivyo si haki suala la mabadiliko ya katiba ya nchi yakafanywa ni maagizo elekezi ya kufuatwa na wananchi na zaidi wanachama wa CCM.
Kwa sasa CCM haina uhalali sio tu wa kuhodhi katiba ya nchi bali hata kutoa agizo kwa umma kwamba wafuate mtazamo wake katika kutoa maoni juu ya katiba mpya. Natambua kuwepo kwa msimamo wa CCM kuhusu wanachama wake kuwataka wakatoe maoni katika Tume ya Jaji Warioba wasema wanataka Serikali mbili!
Hapa leo ndipo hoja yangu itakapojikita,lakini zaidi nitautizama msimamo huo wa CCM kwa upande wa pili wa shilingi kwamba ikiwa kuna wanachama wasiokubaliana na maoni hayo ya ‘kupewa’ nini tafsiri yake? Lakini pia katika nchi huru yenye kufuata misingi ya haki za binadamu kwa kuzingatia katiba ya nchi, haipendezi kuwalazimisha watu kuacha maoni yao kufuata ya Chama au kikundi fulani.
Msimamo wa CCM kuwashurutisha wanachama wake kwenda kusema wanataka Serikali mbili umewanyang’nya haki ya kimsingi ya uhuru wa kufikiri,lakini pia tunaweza kupata katiba mbovu yenye mawazo yanayolingana na hii naweza kuitafsiri kuwa zile nguvu za watawaliwa kuwadhibiti watawala zimeondolewa na kuwa kinyume chake watawala kuwadhibiti watawaliwa.
Watu wafahamu kuwa kama kuna nchi ikaanza kutoa maoni na mapendekezo yake kwa wananchi ili wachangie kwa lengo la kufanyia mabadiliko katiba ya nchi, tambua kuwa katiba inayotaka kutungwa au kurekebishwa ni ya watawala.
Katika hili lazima wananchi na hasa Wazanzibari waelewe kwamba katiba ya nchi inapaswa kuwa ni mali yao na tena inayo mahusiano ya moja kwa moja na maisha yao ya kila siku na kwa muktadha huo ni lazima pia mabadiliko yoyote yaanze kutoka kwao.
Akina Nape Nnauye mnaposema mwana CCM atakayekwenda kutoa maoni tofauti na yaliyobatizwa na NEC ya Chama chenu ni kuviza demokrasia na kuwafanya wanachama wenu uwezo wao wa kufikiri mdogo jambo ambalo mimi siliamini hata kwa mtutu wa bunduki.
Dola ya Tanzania inaongozwa na CCM ni jambo la kustajabisha Chama hicho kinapingana na uamuzi wa Serikali yake katika suala zima la katiba mpya, kwamba Rais Jakaya Kikwete ameunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kupata maoni ya wananchi kuhusu jambo hilo, kama CCM haikuwa ikitaka mawazo tofauti wangeiambia Serikali isiunde Tume.
CCM kuwafunga midomo wanachama wake ni sawa na kuwa na kiungo katika mwili kilichopooza ambacho hakiwezi kufanya jambo lolote kimezidiwa hata na mwana sesele anayetiwa betrii akacheza cheza.
Tunashukuru Mungu kuwa katika Mkoa wa Kusini Unguja si wanachama wa CCM wala wa vyama vyengine waliofuata maagizo elekezi ya vyama vyao, bali wametoa mitazamo yao na ndio maana kwenye ngome ya CCM Kusini Unguja maoni ya kutaka mabadiliko katika mfumo wa muundo wa Muungano yameshika kasi.
Kwa maana nyengine wameyapuuza maagizo elekezi ya Chama chao, hivyo CCM na viongozi wake wanapaswa kujithamini upya maana hali ndio hiyo ule wakati wa ‘zidumu fikra za Mwenyekiti’ umeshapita, hakuna mawazo ya kushikiwa.
Mara nyingi CCM haijifunzi kutokana na makosa yake, kama wangekuwa wanajifunza matokeo ya ripoti ya Jaji Nyalali na Jaji Robert Kisanga wasingekuja na maagizo yasiyotekelezeka kwa wanachama wao maana kwa wakati ule asilimia kubwa walitaka mabadiliko katika Muungano, hawakuchangia maoni kama walivyotakiwa na Chama chao.
Sote tunafahamu matokeo ya ripoti ya Jaji Kisanga, Chama tawala na Rais wake kwa wakati huo Benjamin Mkapa walikuwa wakali na kwa sehemu kubwa walichukizwa na taarifa hiyo kwa sababu ilidhihirisha kwamba si wananchi wala Kamati inayokubaliana na matakwa ya Watawala.
Tunaelezwa kwamba ni wananchi laki sita tu ndio waliochangia maoni na katika hao wapo pia waliopinga moja kwa moja maoni ya serikali, na kubakisha idadi ndogo tu ya wananchi wasiozidi laki nne waliokubaliana na maoni ya Serikali.
Wengi hawakwenda kutoa maoni yao na hii inaweza kusababishwa na mambo mengi,lakini kubwa ni kwamba wananchi hawa ni watu wazima wenye akili timamu hawapendi maoni ya kupewa mkononi, kila mtu yuko huru na hilo limethibitishwa na kupewa nguvu kwenye katiba yetu.
Hatutaki kuamini kwamba haki na demokrasia ni maneno tu yanayotumiwa na Chama tawala ili kuwalaza usingizi mnono wananchi huku wakinyimwa haki yao ya msingi ya kushiriki kutoa maoni wanayoyaona yanafaa.
Wazanzibari wakati umefika sasa tukaachana na ushabiki wa vyama vya siasa tukaendelea na juhudi zetu kudai mabadiliko katika mfumo wa muundo wa Muungano na bila shaka tuungane kufikiria kuhusu mustakbali na hatima ya nchi yetu Zanzibar vyenginevyo, kwa ‘kuiendekeza’CCM itatufikisha ging’ingi.
Hali ya kiuchumi tuliyonayo Zanzibar kwa miaka 48 ni matokeo ya mfumo mbovu wa muundo wa Muungano, sera zake za kiuchumi haziisaidia Zanzibar kuwapeleka mbele katika kuwa na uchumi endelevu na imara, tutaendelea kusambaza bakuli kwa wajomba mwisho watatuchoka.
Kama unalo wazo ambalo unadhani linaweza likaleta manufaa usikae kimya kwa kuhofia tamko la kina Nape, Vyama vya siasa ni vya kupita tu,lakini Zanzibar itaendeela kuwepo, tujiulize viko wapi leo vyama vya siasa kabla ya Mapinduzi?
CCM wasifikiri Wazanzibari wamelala usingizi fofofo, ikiwa wataamini hivyo basi wakae wakijuwa kuwa kioo kimewacheza kizazi cha leo cha Zanzibar sio kile cha mwaka 1964 na kwa kuthibitisha haya tazama maoni yaliyotolewa Mkoa wa Kusini Unguja kuhusu katiba mpya.
Mlalahoi mwenzangu fahamu kwamba unapowasikia viongozi wa CCM, wakihubiri kwamba wametoa mamauzi yale kwa sababu ndivyo wananchi wanavyotaka, kaa ukijuwa wananchi wanaokusudiwa hapo ni vigogo wenziwao, wewe mlalahoi unaeishi Mwakaje, Mikunguni, Fuoni, Darajabovu, Chumbuni huna chako, wewe utapewa wali na pilau, kanga na kikoi na kisha utupwe kwenye mavumbi mpaka baada ya miaka mitano tena ndio ukumbukwe kuja kupewa tena pilau, kanga na kikoi.
Vyama vya siasa kuanza kuwatisha wanachama wake kuwafukuza uanachama ni sawa kuwafanya watumwa ndani ya nchi yao, maana watakuwa si huru kusema yale wanayoyataka, wakitoa maoni tofauti ambayo hayawapendezi Muhafidhina wataanza kutumia rungu la Chama kutisha wanachama.
Kwa tamko la CCM tafsiri yake ni kwamba watu hawana uhuru wala haki ya kutofautiana mawazo. Yeyote anayetofautiana na tamko hilo anahesabiwa kama muasi,mchochezi, msaliti.
Ni jambo la kusikitisha kuona Tanzania baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika na miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar watu wanakosa uhuru ndani ya nchi huru basi hawezi kuendelea hata kama nchi hiyo ingerundikiwa utajiri wote wa dunia, kama leo mtu anafundishwa au anashurutishwa kutoa maoni yasiyoyake na asiyeyaamini hili ni tatizo kubwa katika demokrasia yetu.
Tukumbuke kuwa nchi nyingi zilizopiga maendeleo watu wake walikuwa na uhuru, watu wasio huru hawawezi kusonga mbele kimaendeleo kila siku tukariri kama kasuku maoni ya watu fulani na ndio maana mipango mingi ya maendeleo haitekelezeki kwa sababu haikupangwa na watu wenyewe, imepangwa na wakubwa Serikalini.
Kwa sasa Wazanzibari tuna vipaumbele vyetu katika katiba na zaidi kuliko yote suala zima la Muungano watu wanataka mabadiliko katika mfumo wa muundo wake, wameuchoka muundo wa sasa ambao hauwaletei faida za kiuchumi.
Hivyo basi, suala la kutoa maoni kuhusu katiba mpya kutekwa nyara na tamko la CCM ni kudhihirisha kuwa madai ya wananchi kwamba CCM, wanaelekea kuwa na nia ya kutokuheshimu matakwa ya wananchi katika kuilea na hatimae kuikuza demokrasia ya kweli Tanzania.
Wengi tunaamini kuwa katiba ndio nguzo ya Taifa na pia ndio sheria kuu ya nchi, kwa sababu hiyo, kigezo cha kwanza cha kuthibitisha kama kweli nchi ina muelekeo wa kidemokrasia ni kuonekana kwa misingi ya demokrasia katika mchakato wa utoaji maoni katika Tume ya Jaji Warioba.
CCM inaelekea kutaka kukumbatia utawala wa kiimla, kwa kuwalazimisha watu kusema wanayotaka wao. Watu wa Tanganyika wanayao katika mabadiliko ya katiba, watu wa Zanzibar pia wana mambo yao ambayo jambo la kwanza kabisa ni Muungano.
Je, wanachama wa CCM watabakia kama watu wa kusadiki kila kitu au watafuata wosia wa Mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete aliposema akili za kuambiwa changanya na zako.
---
cross-post kutoka facebook.com/wavuti.nukta77/posts/432232163482734
No comments:
Post a Comment