MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imewekwa matatani ikielezwa kuwa nayo inastahiki kuchukuliwa hatua kutokana na kuzembea katika ukaguzi wa dawa na hivyo kusababisha dawa bandia za kupunguza makali ya ukimwi (ARV’s) kusambazwa.
Sakata hilo linakuja wiki chache tangu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Joseph Mgaya, na viongozi wengine kupisha uchunguzi wa tuhuma za kusambaza dawa hizo.
Wengine waliosimamishwa kazi ni mkuu wa kitengo cha udhibiti ubora na ofisa uthibiti ubora huku kiwanda cha dawa cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) kikisitishiwa uzalishaji na usambazaji wa dawa zilizokwishatengenezwa.
Taarifa za ndani ya TFDA ambazo Tanzania Daima imedokezwa na mmoja wa maofisa wake ambaye aliomba kuhifadhiwa jina kwa vile si msemaji, zilisema kuwa mamlaka hiyo nayo ilizembea katika sakata zima la dawa bandia za ARV’s kusambazwa.
Kiwanda chochote kabla ya kuzalisha dawa au chakula nai lazima kipate kibali cha TFDA baada ya kukaguliwa na kukidhi viwango husika.
“Hata dawa ingekuwa inaingizwa kutoka nje ya nchi, vilevile TFDA inapaswa kukikagua kiwanda husika kuona kama kina ubora wa kutengeneza dawa na kukidhi viwango,” kilisema chanzo chetu.
Gazeti hili pia limefanikiwa kupata nakala ya waraka wa TFDA kuhusu hali ya viwanda vya dawa nchini, ambayo inabainisha kuwa Tanzania ina viwanda saba vya dawa vilivyosajiliwa katika mwaka 2011/2012.
Viwanda hivyo ni Shelys Pharmaceuticals Ltd, Zenufa Laboratories Ltd, Mansoor Daya Chemicals Ltd, Keko Pharmaceuticals (1997) Ltd, Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd, A.A. Pharmaceuticals Ltd na Tanzansino United Pharmaceuticals (T) Ltd.
Waraka huo unabainisha kuwa kiwanda cha Tanzansino United Pharmaceuticals (T) Ltd, ambacho serikali kupitia Jeshi la Kujenga Taifa ni mmbia mmojawapo kimesimamisha utengenezaji dawa tangu Agosti 2010 kutokana na mwekezaji wa nje kujiondoa.
“Ukaguzi uliofanywa na TFDA katika miaka ya fedha ya 2010/11 na 2011/12 umeonyesha kuwa hakuna kiwanda kilichokidhi viwango vya utengenezaji wa dawa,” alisema ripoti yao.
TFDA katika taarifa yake hiyo inakiri kuwa viwanda vya dawa hapa nchini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita vimeshindwa kukidhi vigezo vya usajili wa dawa.
Kutokana na hali hiyo dawa za viwanda hivyo zimekuwa zikiruhusiwa na mamlaka hiyo kuwepo sokoni kwa kuzingatia utaratibu maalumu ambao hauzingatii vigezo vyote vya usajili wa dawa.
“Utaratibu huu ulikuwa wa muda mfupi uliokuwa na nia ya kutoa muda kwa kiwanda husika kurekebisha mapungufu ili dawa zao zisajiliwe. Baadhi ya dawa zinazotengenezwa na viwanda vya ndani ni za tiba za ugonjwa wa malaria na vijiua sumu,” iliongeza taarifa.Via Tanzania Daima.
Pia inafafanua kuwa katika siku za karibuni, sampuli za matoleo (batches) kadhaa za dawa za viwanda hivyo zilizochukuliwa katika soko na kuchunguzwa zimeonekana kuwa na ubora duni na hivyo kuondolewa.
Ni katika mtiririko huo, mtoa habari wetu anasema TFDA haijawahi kutoa kibali kwa kiwanda cha TPI kuzalisha dawa za ARV’s kinachoonyesha kuwa kiwanda hicho kimekidhi vigezo tajwa.
Lakini katika hali inayoonyesha kutokuwepo umakini, TFDA ilizisajili dawa hizo za ARV’s kutoka TPI wakati katika ripoti yake wanakiri kuwa kiwanda hicho hakina sifa za kuzizalisha.
“Dawa inaweza kuwa moja lakini ikawa na matoleo tofauti, hivyo hata toleo hilo la dawa bandia zinazolalamikiwa halikuletwa TFDA kwa ukaguzi maana ingebainika haraka kabla ya kuingia sokoni,” kiliongeza chanzo hicho.
Ofisa huyo anashauri kuwa TFDA ilipaswa kuwa na mkaguzi wake ndani ya MSD ambaye angekuwa anasaidia kukagua na kuhakikisha dawa hizo hazizalishwi na kusambazwa.“Hapa utaona kuwa haikuwa sahihi kumwajibisha mkurugenzi wa MSD pekee na kutuacha TFDA ambao hatukutimiza wajibu wetu. MSD hawana utaalamu wa kuchunguza dawa bandia hiyo ni kazi ya TFDA,” alisisitiza ofisa huyo.
Dawa hiyo bandia aina ya TT-VIR 30 toleo namba OC.01.85 iliyotengenezwa Machi 2011 na kuisha matumizi Februari 2013, nyaraka zake zilionyesha kiwanda cha TPI kiliwauzia MSD.
Waziri Mwinyi alieleza kuwa vidonge vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa husika vilikuwa vimesajiliwa na TFDA.
Mkurugenzi Mkuu wa TFDA jana alipotafutwa kwa njia ya simu, alisema atatoa ufafanuzi wake leo akiwa ofisini.
No comments:
Post a Comment