WATOTO watano wamefariki dunia kwa kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu katika kijiji cha Ihanda maeneo ya Rugalama wilayani Karagwe, mkoani Kagera.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa, Philipo Karagi, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa tano asubuhi wakati watoto hao wakichezea mabaki ya chuma chakavu kilichokuwa kikipimwa.Kamanda Karagi aliwataja watoto waliopoteza maisha kuwa ni Thenias Frank (miaka mitatu), Faraja Frank (mwaka mmoja), Nelson Alphonce (17) ambaye ni mwanafunzi aliyemaliza darasa la saba mwaka huu, Edgar Gidion na Skaeus Kamali (12).
Alisema chanzo cha tukio hilo ni kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Evadius Kiloba (15) ambaye anasubiri majibu ya mtihani wa darasa la saba. Baada ya kumaliza mtihani huo, amekuwa akifanya kazi ya kukusanya vyuma chakavu ambavyo anavirundika katika eneo hilo huku akiuza kwa wateja wanaojitokeza.
“Baada ya kukusanya vyuma hivyo katika eneo hilo, watoto walianza kuchezea baadhi ya vyuma kikiwemo kitu hicho kinachosemekana ni bomu ambalo lililipuka na kuua watoto hao,” alisema Kamanda Karagi na kuongeza kuwa mtoto mmoja kati ya waliojeruhiwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Kamanda Karagi, alisema ilipofika majira ya saa 5:00 asubuhi ndipo kuliposikika mlipuko na hivyo kulazimu jeshi la polisi na kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi ili kuchunguza mlipuko huo.
Alisema baada ya wataalamu kufanya uchunguzi wa kina, walibaini kuwa bomu hilo ni la kurushwa kwa mkono. Alisihi wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa na kuacha kugusa vitu ambavyo wanavitilia shaka.Habari na Betty Kangonga.
No comments:
Post a Comment