MSAIDIZI wa ndani, Doyi Yusuph (13), mwenyeji wa mkoa wa Kigoma,
anasadikiwa kuiba mtoto wa kike, Yasinta Joel (5), katika nyumba
aliyokuwa akifanya kazi wilayani Bukombe, Geita, na kisha kutoweka naye
kusikojulikana.
Akizungumza juzi, bibi wa mtoto huyo, Perepatua
Alphonce, alisema dada huyo amefanya wizi huo huku akiacha sanduku lake
la nguo, jambo ambalo liliwahadaa kwa kutogundua haraka kitendo hicho.
Perepetua maarufu kwa jina na Bibi Mgaya, alisema mjukuu wake huyo
alikuwa akisoma chekechea kwa Mwalimu Kapesa na alikuwa akiishi na babu
yake, Edward Mgasa.
Alisema dada huyo ambaye alikuwa na wiki moja tangu aanze kazi katika
familia ya Mzee Mgasa, alimuiba mtoto huyo Novemba 23, mwaka huu, majira
ya saa tatu asubuhi. Wakati akiondoka naye mtoto huyo alikuwa amevaa
blauzi ya maua yenye mchanganyiko wa rangi nyekundu na zambarau na sketi
ya Jeans rangi ya bluu.
“Niliishaachana na Mzee Mgasa ambaye alioa mke mwingine na walikuwa
wakishirikiana kumlea mjukuu wetu. Siku ya tukio mzazi mwenzangu alikuwa
kwenye machimbo madogo ya Ng’anzo kwenda kutafuta riziki,” alisema
Perepetua.
Alisema amesharipoti suala hilo katika kituo cha polisi cha wilayani
Bukombe na kufunguliwa jalada namba USH/IR/177/2012 na kuwaomba raia
wema wanaomuona mtoto huyo kutoa taarifa katika kituo chochote cha
polisi au kuwasiliana naye kwa simu namba 0755 910 377.
No comments:
Post a Comment