Awali ya yote naanza kwa kutoa mkono wa pole kwa wapenda burudani kote
nchini kutokana na misiba ya wasanii iliyofuatana, jambo lililoipelekea
kuwa na majonzi yasiyokoma.
Awali alianza Maria Khamis ‘Paka Mapepe’ aliyekuwa muimbaji wa muziki
wa taarab wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT) aliyefariki kutokana
kifafa cha uzazi.
Wakati watu wakiwa hawajakaa sawa wala machozi kufutika vema usoni au
kwa msemo mwingine naweza kusema ikiwa bado tanga halijaanuliwa sawasawa
tasnia ya filamu ikaondokewa na Khalid Mohamed a.k.a Mlopelo (41)
aliyeng’ara na kikundi cha Kaole kilichokuwa kikirushwa na kituo cha
televisheni cha ITV ambako ndiko alikopata umaarufu wake na hatimaye
kushirikishwa katika filamu kadhaa.
Wakati msiba wa Mlopelo haujaisha msanii mwingine wa Bongo Movie
John Maganga akafariki Jumamosi iliyopita na kuzikwa Jumanne wiki hii.
Wakati kukiwa kuna msiba wa Maganga Jumatatu usiku msanii Ramadhan
Mkiteti alipata ajali maeneo ya Maguzoni Muheza mkoani Tanga.
Hakika wasanii na tasnia wamekumbwa na misiba yote ya uchungu; nachukua fursa hii kuwapa pole.
Ni kweli hakuna msiba unaozoeleka hata siku moja kama babu au bibi yako amefariki miaka kadhaa iliyopita, inauma sana.
Kama hiyo haitoshi hata kwa sisi tuliopoteza wazazi wetu kama mimi
ambaye sina mama kwa kweli ninaposikia habari ya msiba huumia sana na
kunitonesha machungu ambayo ninayo wakati wote.
Vivyo hivyo napenda kuwapa pole wafiwa hasa mama Mlopelo, Mama Sharo
Milionea na wazazi wa Maganga kuwa wamshukuru Mungu kwa yote.
Nikiwa nyumbani kwangu ambapo nilifuatilia kipindi cha ‘Take One’
kinachorushwa na televisheni ya Clouds nilimsikia baba mdogo wa
marehemu Maganga aliyejitambulisha kwa jina la Deogratius Shija
akibainisha kwamba kifo cha mtoto wao kilitokana na uzembe wa wasoma
vipimo X-Ray ambapo wao walipofika katika Hospitali ya Mwananyamala
walilazimika kupiga picha ili tatizo libainike.
Ndipo iliposomeka kwamba alikuwa na tatizo la kutoboka utumbo hivyo
akatakiwa kufanyiwa upasuaji na akafanyiwa upasuaji lakini hali yake
haikutengemaa.
Maskini pindi alipopewa uhamisho wa kwenda kutibiwa katika hospitali
ya taifa ya Muhimbili (MNH), ambako ndiko kwenye mashine kubwa za kuweza
kumsaidia kupumua akiwa huko ndipo akapatiwa vipimo vingine nao
wakagundua kwamba bandama lilipasuka hivyo upasuaji aliofanyiwa katika
Hospitali ya Mwananyamala ulifanyika kwa makosa.
Kama hiyo haikutosha tabibu bingwa wa magonjwa hayo alikuwa amemaliza
muda wake wa kazi hivyo ndugu wakaambiwa wasubiri hadi ambapo
angeliingia kazini kesho yake.
Ikumbukwe kwamba wakati huo marehemu Maganga alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine hospitalini hapo.
Lakini hadi tabibu anafika alfajiri hali haikuwa nzuri kwani hata
upumuaji wa mgonjwa ulikuwa wa taabu licha ya kusaidiwa na mashine.
Inasikitisha na inauma sana jinsi hali ilivyo na kifo cha Maganga kilivyotokea ni uzembe mtupu.
Jamani mbona hali inatisha kwenye hospitali zetu za serikali? Kwa
nini iwe ni wao tu kila mara ni Mwananyamala tu? Hebu wahusika tupieni
macho suala hili.
Waangaliwe wasoma vipimo na hata huyo tabibu na jopo lake waseme wazi
kama kweli walipomfanyia upasuaji ni kweli walikuta utumbo umetoboka
kwani hapa hakuna anayeweza kusema mkweli ni nani. Hivi wizara husika
haisikii kadhia zote hizi zinazowakuta wananchi wake?
Nimeguswa na sana na vifo hivi huku kila mmoja akiwa na sababu yake
iliyosababisha afe lakini sababu ya Maganga ni uzembe wa baadhi ya
matabibu wetu hawakuwa makini kuanzia hatua ya awali.
Huenda wakati mwingine inawezekana ikawa ni uchakavu wa vifaa vya hospitalini kwetu lakini kwa nini iwe hivyo?
Jambo lingine lililonishtua ni kusikia kwamba walishindwa kumwekea
mashine ya kupumua kwa sababu iliyopo katika Hospitali ya Mwananyamala
haina nguvu hivi ni wagonjwa wangapi wanaopoteza maisha yao hospitalini
pale?
Kumbe Mwananyamala kuna siri tena nzito ambayo imefichuliwa na kifo
cha Maganga; siri hii ni kumsababishia maumivu makali yaliyosababisha
kifo chake, walimkata utumbo pasi na sababu ya kufanya hivyo ilhali ana
tatizo lingine na mashine zao hazina nguvu.
Huu ni ukatili kwa baadhi ya watendaji wa serikali kwa kutokuwa makini
na kujali wananchi wake ambao wanakufa kwa kulazimishwa kwa matibabu
yasiyokidhi na vifaa duni.
Na ni serikali hii hii itakayokaa kimya bila kulitolea ufafanuzi
suala hili. Inasikitisha imekuwa ni mazoea sasa kwani historia ya
matabibu wasiozingatia weledi inazidi kuandikwa, walipasuliwa wagonjwa
kichwa badala ya mguu na mguu badala ya kichwa serikali hiihii ilikaa
kimya.
Ndugu wa wagonjwa walishtaki hasa yule aliyepasuliwa kichwa kwani tayari amepewa ulemavu asiokuwa nao.
Vivyo hivyo kama mapenzi ya Mungu yasingetimia kwa kumchukua Maganga
ina maana na yeye tayari alikuwa amepewa ulemavu wa utumbo wake na je
angeishi vipi katika hali ile endapo yasingemkuta mauti?
Majibu ya hayo yote yanabaki kwa kila mmoja kujitafakari na kuchukua hatua.
Poleni wafiwa wote kwa yote yaliyowakuta; ni mapenzi yake, kila nafsi
lazima itaonja mauti sawa lakini mauti nyingine husababishwa na baadhi
ya matabibu wasiokuwa makini na kazi zao.
Huu ni mtazamo tu kwenu matabibu na wauguzi wala msiniwekee chuki.
No comments:
Post a Comment