Na Salum Mkandemba wa Tanzania Daima.
WAKATI malalamiko kwa waamuzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuhusu
kuboronga yakishika kasi, Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Saad Kawemba, amewakingia kifua na kudai uamuzi wa haki
zaidi ya walioutoa haupatikani duniani.
Akizungumza na kipindi cha Tuongee Asubuhi – Michezo, kinachorushwa na
kituo cha Star TV cha jijini Mwanza kila siku za Alhamisi, Kawemba
alisema kuwa kamati yake imeridhishwa na kiwango cha uchezeshaji cha
waamuzi hao, licha ya kukiri kuwapo kwa kasoro kadhaa, akidai ni za
kibinadamu.
Kawemba alisema kuwa waamuzi kama walivyo binadamu wengine, hawawezi
kufanya uamuzi wa kumfurahisha kila mmoja, huku akidai, kutovunjika
mechi yoyote kutokana na uamuzi wao, ni uthibitisho mwingine kwamba
walikuwa makini katika mechi hizo.
“Niseme ukweli kiwango cha uchezeshaji wao kilikuwa kizuri na
kimetuvutia. Najua wapo ambao hawakupendezwa nayo, lakini ndivyo
binadamu tulivyo. Haki ya kiwango hicho hupatikana mbinguni, sio
duniani,” alisema Kawemba aliyekuwa akizungumzia usajili wa dirisha dogo
Januari mwakani.
Kawemba alisema kuwa hatua kali kwa waamuzi wabovu na wazembe
zilizochukuliwa mapema mwanzoni mwa msimu huu wa 2012/13, zilisaidia
kuongeza umakini miongoni mwao, kiasi cha kuimarisha utendaji wao
dimbani hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.
Akaenda mbali zaidi na kukosoa kauli za makocha wa klabu za Ligi Kuu,
juu malalamiko yao kuwa viwanja vibovu mikoani ndiyo chanzo cha matokeo
mabovu ya timu zao na kuwataka kufanya tathmini za matokeo chanya pindi
zinaposhinda na sio kutathmini matokeo hasi tu.
“Sisi kama TFF tunaishukuru sana serikali kwa kukubali kutupa Uwanja
wa Taifa kwa matumizi ya Ligi Kuu. Haiwezekani viwanja vyote vikawa kama
ule, fursa tuliyopata ya kuutumia, isiwalemaze baadhi ya makocha kiasi
cha kutarajia viwanja vyote nchini kuwa kama Taifa,” alisaema.
Katika mzunguko wa kwanza uliofikia tamati hivi karibuni, kilio
kikubwa kilikuwa ni kuvurunda kwa waamuzi wa Ligi Kuu, kulikotokana na
ama kushindwa kutafsiri sheria au upindishaji wa kawaida, utokanao na
mapenzi au rushwa, kitu kilichothibitishwa na kuondolewa au kufungiwa
kwa baadhi yao.
Baadhi ya waamuzi waliokumbana na adhabu za kufungiwa, kuondolewa au
kuonywa katika Ligi Kuu kutokana na kuvurunda ni pamoja na Mathew Akrama
na Paul Soleji wa Mwanza, Ephraim Ndissa, Mwarabu Mumbi, Ronald Swai na
Kamishna Pius Mashera.
No comments:
Post a Comment