Wakizungumza na Tanzania Daima nje ya ofisi za Jiji la Arusha wakati wakisubiri kuonana na Meya Gaudensi Lyimo, walisema kuwa, kitendo kilichofanywa na waandaaji wa shughuli hiyo kumwalika Diamond na kuwaacha wasanii wa Arusha katika sherehe hizo ni dharau kubwa kwao.
Akizungumza kwa niaba ya wasanii hao, Mwenyekiti wa wasanii hao, Hussein Sichonge, alisema kuwa, wao kama wasanii wakazi wa Arusha, wamefedheheshwa sana na kitendo hicho.
“Tumefedheheshwa sana na kitendo hiki, yaani viongozi hawa ambao huchukua kodi zetu sisi wakazi wa Arusha, wanaamua kuzipeleka kwa msanii wa Dar es Salaam, eti aje kutuburudisha wakati wa kutuzindulia jiji letu sisi ambao ndio tumechangia kulifikisha hapa, ni fedheha kubwa,” alisema Sichonge.
Alifafanua kuwa, baada ya kukutana na kutafakari, wakaamua kufika katika ofisi hizo kukutana na meya, ambaye ndiye mwenye dhamana ili kuwasilisha malalamiko yao hayo ya msingi ili ajue kimewaumiza sana.
Alisema wao kama wasanii, walitegemea ndio wangetakiwa kupewa jukumu hilo, ambako kwa umoja wao, wangeamua kutunga wimbo maalum kwa ajili ya sherehe hizo kuhusiana na Arusha.
“Sasa leo imebaki siku moja kabla ya shughuli yenyewe ndiyo tunajua, wakati wasanii wa Dar es Salaam walishafanyiwa mpango huu mapema na kujiandaa, ikiwemo kulipwa kabisa fedha nyingi kwa ajili ya kazi hii, ambayo ingeweza kufanywa na wasanii wa Arusha,’’ alisema Sichonge.
Naye Nakaaya, alisema kuwa, Arusha kuna wasanii wakubwa wa ndani ya nchi na nje, ambao wanathaminika sana hapa nchini, lakini kitendo kilichofanywa kutowashirikisha na kuamua kumuita msanii kutoka Dar es Salaam ni kuwadhalilisha kisanii.
Akizungumzia malalamiko hayo, Meya Lyimo licha ya kukiri upungufu huo, alisema atahakikisha wanalishughulikia suala hilo na wasanii wa Arusha kupata heshima yao katika shughuli hiyo ya uzinduzi leo.
Shughuli ya uzinduzi wa Jiji la Arusha, inafanyika leo, ambayo itaongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye atahutubia katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mara baada ya uzinduzi utakaofanyika katika mnara wa Mwenge, majira ya saa sita mchana.
Chanzo:daima
No comments:
Post a Comment