WANANCHI wa Njiro jijini hapa wamedai kuwa wako hatarini kupata maradhi ya saratani kufuatia hatua ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanaesco) kubadili matumizi ya ardhi ya eneo walilokuwa wakilitumia kusambaza umeme na kulitoa kwa kampuni ya Symbion Power (T) Ltd kufua umeme.Aidha wamedai kuwa TANESCO hawajafanya tathmini ya athari za mazingira kama sheria inavyoagiza.
Wananchi hao kutoka vitalu B, C, na D wanadai kuwa mitambo mikubwa iliyofungwa kwenye kitalu C inayozalisha megawati 66 inasababisha kelele, mitikisiko inayosababisha nyufa kwenye nyumba zao, moshi wenye kemikali unaosababisha uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha usalama wa afya zao.Tayari wananchi hao wamefikisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, kwa barua iliyosainiwa kwa niaba yao na wananchi sita tokea Septemba 4 mwaka huu lakini wanadai kuwa licha ya mkuu huyo kuahidi kushughulikia suala hilo, hawaoni mabadiliko yoyote.
Mmoja wa wananchi hao, Gelase Rutachubira, aliieleza jana kuwa walimuomba mkuu wa mkoa achukue hatua za haraka ikiwemo kusimamisha shughuli kwenye eneo hilo ili kunusuru afya na makazi yao.Kwa upande wake Mulongo alikiri kupata malalamiko hayo ambapo alisema kuwa kuyashughulikia ina maana awaagize TANESCO kusimamisha uzalishaji huo wa umeme jambo alilodai kuwa hana uwezo nalo kwani kwa sasa nchi inahitaji nishati hiyo ya umeme.
Alisema anachoweza kufanya ni kukutana na uongozi wa TANESCO kuona namna wanavyoweza kuboresha shughuli zao kwa kutumia teknolojia nyingine itakayowezesha kuzuia kelele, mitikisiko na uchafuzi wa hewa hata hivyo alidai kuwa shughuli kwenye eneo hilo hazifanyiki muda wote wa siku.
Aidha barua nyingine toka Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini (NEMC) yenye kumbukumbu namba NEMC/ 513/Vol 1/148 ikimjibu mwananchi wa eneo hilo, Method Mukurasi, aliyelalamikia kampuni hiyo ilidai kuwa tathmini ya mazingira kwenye eneo hilo ilikuwa bado haijafanyika hivyo wangefika kwenye eneo hilo kwa ajili ya kuifanya na wangempa taarifa.Hata hivyo juhudi za kumpata msemaji wa TANESCO kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba kutokana na simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.Habari na Grace Macha, Arusha.
No comments:
Post a Comment