Chanzo cha habari-Tanzania Daima.
LICHA ya viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini
pamoja na wale wa Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO), kujaribu kuficha
ukweli kuhusu hali ya uzalishaji na usambazaji wa umeme wa uhakika
nchini, Tanzania Daima imedokezwa kuwa hali ni tete.
Kutokana na mkakati wa wizara husika ulivyo sasa, inaelezwa kuwa ili
mgawo wa umeme utoweke, kiasi cha sh bilioni 42 zitapaswa kutumika kila
mwezi kwa ajili ya kuyalipa makampuni yanayoiuzia TANESCO umeme.
Kwa muda mrefu sasa TANESCO imeelezwa kuwa hoi kifedha licha ya kuwa
na makusanyo makubwa lakini fedha hizo zimekuwa zikiishia mikononi mwa
mafisadi na hivyo shirika hilo kubakia tegemezi kwa serikali.
Kwa mujibu wa takwimu za Waziri wa Naishati na Madini, Prof. Sospeter
Muhongo, alizozitoa bungeni wakati akihitimisha hoja ya hotuba ya bajeti
yake kwa mwaka 2012/2013, TANESCO inakusanya mapato kati ya sh bilioni
60 mpaka 70 kwa mwezi.
Hata hivyo katika hali ya kushangaza, licha ya matumizi ya shirika
hilo kuwa sh bilioni 11 kwa mwezi, Waziri alishindwa kufafanua ni wapi
zinakwenda sh takribani bilioni 40 zinazosalia.
Waziri Muhongo alilieleza Bunge upotevu huo wa mabilioni bila
kufafanua Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya
Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), wamefanya nini kama fedha hizo
zinaibiwa.
Wakati hali ikiwa hivyo, Muhongo amenukuliwa akikanusha kuwa hakuna
mgawo wowote wa umeme kwa sababu TANESCO imejipanga kutafuta vyanzo
vingine vya kuzalisha umeme wa uhakika.
Alisema suala la umeme kukatika kwa dakika mbili au tatu si mgawo bali ni kutokana na miundombinu ambayo imechakaa.
Kauli ya waziri haipishani na ile ya naibu wake, George Simbachawene,
ambaye alizungumza na gazeti hili jana akisema wanachodhibiti sasa ni
uzalishaji wa umeme ili umeme uwepo.
Alipobanwa afafanue ni kwa nini umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara
maeneo tofauti nchini, naye aliungana na waziri wake kusisitiza kuwa ni
ubovu wa miundombinu na kwamba huo si mgawo.
Tanzania Daima ilitaka kufahamu miundombinu hiyo itaimarika lini
wakati TANESCO iko hoi kifedha kutokana na kuelemewa na madeni ya
makampuni yanayoliuzia umeme, lakini naibu waziri alijitetea akisema
kuwa kazi yao kama wizara sasa ni kuhakikisha umeme upo.
Licha ya wizara kujaribu kukwepa, gazeti hili limedokezwa kuwa katika
kila sh 100 ambazo TANESCO inakusanya, sh 86 zinakwenda kulipa madeni ya
mikataba iliyosainiwa kifisadi ya Aggreko, Symbion, Songas na IPTL.
Kwa mujibu wa chanzo chetu ni kwamba mpaka sasa Symbion inalipwa sh
milioni 152 kila siku kama gharama za uendeshaji wakati IPTL inalipwa sh
bilioni tatu kila mwezi na Songas sh bilioni 4.5.
“Agrreko wanaiuzia TANESCO umeme kwa senti dola 42 kwa unit moja
halafu TANESCO inauza umeme huo kwa senti dola 11 kwa unit moja,”
kilisema chanzo chetu.
Serikali hii ambayo inababaika sasa kuhusu upatikanaji wa uhakika,
ilikataa ushauri wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA),
wa kuinunua mitambo ya Dowans wakati huo ikiuzwa kwa dola milioni 59 kwa
madai kuwa sheria ya manunuzi ya umma inakataza.
Lakini mitambo hiyohiyo ilinunuliwa baadaye na Symbion kwa dola
milioni 159 na sasa kampuni hiyo inazalisha umeme na kuiuzia TANESCO.
Akizungumzia sakata hilo, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John
Mnyika, alisema kuwa kauli ya waziri na wasaidizi wake haielezi ukweli
kamili kuhusu hali tete ya umeme kutokana na kususua katika utekelezaji
wa Mpango wa Dharura wa Umeme kama nilivyohoji bungeni Julai 27, 2012.
“Kwa mujibu wa nyaraka nilizonazo za ndani ya Wizara ya Nishati na
Madini na TANESCO hali ya uzalishaji na usafirishaji na usambazaji wa
umeme bado ni tete kwa sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa upatikanaji
wa mafuta na gesi asili kwa ajili ya uendeshaji wa mitambo ya kufua
umeme,” alisema.
Alisema kuwa serikali ina upungufu ya fedha za kununua mafuta mazito
ya kuendeshea mitambo ya umeme, hivyo inapaswa kurejea katika
mapendekezo yake aliyoyatoa bungeni Agosti 2011.
“TANESCO inakabiliwa na ufisadi na uzembe unaoongeza gharama za
uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa upande mmoja na
uendeshaji wa shirika kwa upande mwingine.
“Ufisadi na uzembe huo unapunguza uwezo wa TANESCO kuhakikisha
upatikanaji wa umeme wa uhakika na unaongeza gharama na bei ya
upatikanaji wa umeme hali inayoathiri uchumi wa nchi na maisha ya
wananchi,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa nchi haina Kamati ya Bunge ya Nishati na
Madini ambapo wizara ingelazimika kueleza ukweli kamili na halisi, hivyo
amtaka Spika arejee barua yake hiyo na atumie madaraka na mamlaka yake
kwa mujibu wa kanuni ya 116 na kanuni ya 114 fasili ya 14 kukabidhi
suala hilo lishughulikiwe na kamati nyingine.
“Nitakabidhi sehemu ya nyaraka nilizonazo kwa Kamati ya Kudumu ya
Bunge itakayoelekezwa na Spika kushughulikia jambo hili lakini iwapo
hatua za haraka hazitachuliwa mpaka Januari 30, 2013 nitatoa baadhi ya
nyaraka hizo kwa vyombo vya habari na umma,” alisema.
No comments:
Post a Comment