SIKU moja baada ya padri wa kanisa Katoliki lililoko Mpendae
visiwani Zanzibar, Ambrose Mkenda, kujeruhiwa kwa risasi na watu
wasiojulikana nje ya nyumba yake wakati akitoka kanisani, Sheikh wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, amelaani tukio hilo na kuwataka
Watanzania kuwafichua wale wote waliohusika katika tukio hilo baya kwa
mustakabali wa taifa.
Akizungumza jana, Sheikh Salum alisema hivi sasa
kumekuwa na viashiria vinavyonekana kutaka kutowesha amani, jambo
linalohitaji kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja ili kuhakikisha amani
inaendelea kudumu.
Alisema ni muhimu Watanzania wakawafichua wale wote waliohusika katika
tukio hilo, ili kujua ukweli na kuweza kulisaidia Jeshi la Polisi.
“Ni muhimu kujua ukweli wa tukio hili, kwani wapo wanaoweza kuamini kuwa ni viashiria vya chuki vya kidini,” alisema.
Alisema mauaji ya kimbari yaliyojitokeza katika baadhi ya nchi
nyingine za Afrika yalichangiwa na vitu mbalimbali ikiwemo matatizo ya
udini, ukabila vitu ambavyo vimeanza kujitokeza nchini.
Sheikh Salum alisema mfumo wa kukubali ukabila huku wengine wakinyimwa
haki inaweza kuwa chanzo cha kutokea kwa vurugu, hivyo kuna haja ya
kushirikiana kwa umoja, ili kukomesha viashiria hivyo.
No comments:
Post a Comment