CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeeleza
kusikitishwa kwake na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuingilia mamlaka ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mshangao huo wa CHADEMA unatokana na hotuba ya mwisho wa mwaka jana ya Rais Kikwete aliyoitoa jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema Rais Kikwete hakupaswa kutangaza
ratiba na taratibu zingine za
Tume ya Katiba wakati yeye sio msemaji wa
tume hiyo.
“Rais amesema kuwa kwa sasa tume imemaliza hatua ya kwanza ya kuchukua
maoni toka kwa mwananchi mmojammoja, na kaeleza ratiba yote ya tume
tangu Mwezi Mei mwaka 2013, kutakuwa na mapitio ya Rasimu ya Katiba
Mpya, Juni hadi Agosti-tume itakuwa inashughulika na Mabaraza ya Tume na
Novemba utakuwa mwezi wa Bunge Maalumu.
Amepata wapi mamlaka ya
kuisemea tume?” alihoji Mnyika.
Mnyika alisema kuna maeneo mengi nchini ambayo watu bado hawajatoa
maoni, hivyo CHADEMA inashindwa kuelewa hatua hiyo ya Rais Kikwete
kuutangazia umma kwamba tume imemaliza kazi yake ya awamu ya kwanza.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, ameitaka Ikulu itoe tamko lini
Rais amekuwa msemaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwani kwa kufanya
hivyo ameingilia kati mamlaka ya tume.
Kwa mujibu wa Mnyika, hatua hiyo ya Rais Kikwete imethibitisha hofu ya
muda mrefu kwamba tume hiyo sio huru na inafanya kazi kwa maelekezo ya
Rais.
“Tunashindwa kuelewa Rais ameenda mbali zaidi hadi kuzungumzia
mabaraza yatakayoundwa kwa ajili ya kupitia rasimu na maoni ya wananchi,
wakati hata sheria yenyewe iliyotungwa iko kimya kuhusu muundo wa
mabaraza,” alisema Mnyika.
Mbali ya kumlalamikia Rais Kikwete, Mnyika alisema CHADEMA imesisitiza
kuwa mwaka 2013 utakuwa wa nguvu ya umma ambapo wataishinikiza serikali
kuwajibika kwa wananchi.
Akizungumzia kuhusu usalama wa nchi, Mnyika alisema kuwa CHADEMA
imemshangaa
Rais Kikwete kutoonyesha kusikitishwa na mauaji yenye sura
ya kisiasa ambapo walishamwandikia barua wakimtaka aunde tume ya
kimahakama ya kijaji ili ukweli kuhusu mambo hayo uwekwe wazi.
“Kitendo cha Rais kumalizia hotuba ya mwisho wa mwaka bila kuchukua
hatua kama ilivyopendekezwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
zinathibitisha pengine Rais hajaisoma ripoti hiyo japo tume hiyo ni
chombo cha serikali na pia amedharau barua ambayo CHADEMA ilimwandikia
hivyo tunawapelekea wananchi waamue, maana hii ni serikali yao,”
alisema.
Zaidi ya hayo, Mnyika pia alitoa msimamo wa CHADEMA kuhusu kuboreshwa
kwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo alisema Rais Kikwete
hajasema lolote kuhusu daftari hilo ambalo halijaboreshwa tangu mwaka
2010.
Alisema hatua hiyo imesababisha Watanzania wengi kupoteza haki yao ya
kupiga kura, hivyo CHADEMA imetoa wito wa kuitaka serikali itoe tamko
lini itaanza kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mwaka huu ili
uboreshwaji huo usaidie katika mchakato wa Katiba mpya.
Pia alielezea kuhusu mjadala mpya ulioibuka hivi karibuni kuhusu ujenzi wa bomba la gesi toka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Alisema ingefaa serikali iwaeleze Watanzania wamenufaika kiasi gani
toka mwaka 2004 bomba hilo la gesi toka Songosongo hadi Dar es Salaam
kuliko kushinikiza kujenga bomba jingine.
Awali katika barua ambayo CHADEMA walimwandikia Rais Kikwete,
walimtaka achukue hatua, kwa mujibu wa mamlaka yake Kikatiba kuhusu
mauaji ya kisiasa.
Pia ilimtaka Kikwete achukue hatua ya kuwafukuza kazi baadhi ya viongozi.
“Tunataka Rais achukue hatua za utekelezaji kwa mujibu wa mamlaka yake
na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ilieleza
sehemu ya barua hiyo.
Waliotakiwa kufukuzwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk.
Emmanuel Nchimbi, IGP Saidi Mwema, Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la
Polisi, Paul Chagonja, RPC wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shigolile, na
RPC wa Iringa, Michael Kamuhanda, kwa kutowajibika kufuatia mauaji.
“Ili kupata ukweli wa sababu za vifo hivyo, mauaji yote haya
hayajafanyiwa uchunguzi wowote wa kimahakama/kijaji kwa mujibu wa sheria
za nchi yetu kinyume na ahadi ya waziri mkuu bungeni wakati
akihitimisha hoja yake katika Bunge la Bajeti la mwaka 2011/2012.
“Hakuna uchunguzi wa kifo ‘inquest’ uliofanyika na hakuna Mahakama ya
Korona ‘Coroner’s Court’ iliyoanzishwa ili kuchunguza vifo hivi,”
alisema Mbowe.
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment