Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibuka na mkakati mpya
wa kushika hatamu za dola katika uchaguzi, baada ya kutangaza kufanya
mabadiliko makubwa ya uongozi na utendaji wake kwa kupeleka mamlaka ya
makao makuu ya chama kwenye kanda 10; nane zikiundwa Tanzania Bara na
mbili visiwani Zanzibar.
Mkakati huo, ambao ni sehemu ya utekeyake ya majimbo, ulitangazwa na
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alipofungua mkutano wa
dharura wa Baraza Kuu la Chama hicho, jijini Dar es Salaam jana,
ulioitishwa kwa lengo la kujadili mikakakti ya uendeshaji wa shughuli za
chama kwa ajili ya mustakabali wa chama.
Alisema uamuzi huo umefikiwa ili kuondokana na mazoea yaliyopo
serikalini ya kung’ang’ania kila kitu kufanywa na kikundi cha watu
wachache jijini Dar es Salaam.
Alisema Chadema imeamua kuuvunja mwiko huo kwa kuwa ni chama, ambacho
kinathaminiwa na Watanzania wote, hivyo akawataka wanaChadema kuishi kwa
kauli zao.
“Kwa hiyo, madaraka ya chama yanatoka makao makuu sasa yanakwenda kwenye
kanda. Chama kimekua. Ukienda kila mkoa kipo. Hatuwezi kung’ang’ania
Dar es Salaam tu. Chama sasa kipelekwe kwenye kanda zenu,” alisema Mbowe
na kuongeza:
“Baada ya kazi kubwa iliyofanywa na makao makuu (ya Chadema) kwa miaka
20, lazima kama chama siasa tujipange kama dola. Tunakwenda kutawanya
chama kwenye kanda 10. Tunakwenda na vikosi 10. Tutapeleka magari,
pikipiki.”
Alisema kazi ya kuchukua dola si ya Mbowe wala ya (Makamu Mwenyekiti wa
Chadema Tanzania Bara, Said) Arfi) peke yake, bali ni ya wote.
Alizitaja kanda hizo kuwa ni Ziwa Magharibi, ambayo itahusisha mikoa ya
Mwanza, Geita na Kagera); Kanda ya Ziwa Mashariki (Mara, Simiyu na
Shinyanga) na Kanda Magharibi (Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa).
Kanda nyingine ni ya Kati (Singida, Dodoma na Morogoro); Kanda ya Nyanda
za Juu Kusini (Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma); Kanda ya Kusini (Lindi
na Mtwara) na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam na Pwani). Nyingine ni
Kanda ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara); Kanda ya
Pemba (mikoa yote ya Pemba) na Kanda ya Unguja (mikoa yote ya Unguja).
Alisema katika kila kanda kutakuwa na ofisi na kwamba, chama kitagawa
vitendea kazi vyote muhimu, yakiwamo magari na pikipiki ili kurahisisha
na kufanikisha shughuli za chama.
Mbowe alisema kila kanda ina maofisa wenye uzoefu wa kukisimamia chama
na zitajumuisha pia wabunge wa maeneo husika. Alisema wamefikia uamuzi
huo ili kukataa malalamiko, ambayo yamekuwa yakitolewa muda mrefu kuhusu
kila kitu kufanywa na makao makuu ndiyo maana wameamua kuyashusha chini
mamlaka yake.
Mbowe alisema sababu nyingine, ni kujipanga kwa ajili ya uchaguzi,
kuanzia ule mdogo wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na uchaguzi
mkuu na pia kudhibiti wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupita bila
kupingwa katika uchaguzi.
“Tatizo kubwa la nchi hii ni watu kukaa makao makuu wakifikiri kuwa
wanajua kuliko wote, wanajua mali kuliko wengine,” alisema Mbowe.
Alisema yanayotokea mkoani Mtwara ni mwanzo unaoashiria kwamba, wananchi
hawana imani na serikali na kusema jambo hilo la kujisifu, lakini
linastahili kupongezwa kutokana na ujasiri unaoonyeshwa na wananchi wa
mkoa huo.
Mbowe alisema msimamo wa Chadema kuhusu gesi ya Mtwara, iko pamoja na wananchi.
“Kama CCM wanafikiri ngoma imeishia Mtwara wangoje, kama ni noma na iwe
noma. Wajiandae kutoa majibu kuhusu dhahabu, mafuta, uranium, twiga,
pembe za ndovu na rasilimali za nchi,” alisema Mbowe.
Aliitaka serikali kusitisha mara moja mpango wa kuisafirisha gesi kutoka
Mtwara kwenda Dar es Salam hadi hapo itakapokaa na wananchi, wajadili,
waridhie na suala hilo lifanyike kwa maslahi ya wote.
Aliitaka pia serikali kuiweka hadharani mikataba yote 26 ya gesi.
Alisema Chadema hawawachukii wawekezaji, lakini wanachohitaji ni wananchi na wawekezaji kila mmoja kufaidi rasilimali za nchi.
Mbowe alisema watu, ambao Chadema ina ugomvi nao ni viongozi waliofungua
milango na kuruhusu wawekezaji wasiokuwa na uwezo kuja kuwekeza nchini.
Kuhusu Katiba aliitahadharisha Tume ya Mabadiliko ya Katiba na serikali
akisema kama wanajidanganya kuwa watakuja kuwapandikizia katiba
wanayoitaka, nchini “hapatatosha”.
“Kama haitakuwa na maslahi ya Watanzania tunaikataa. Kuandika katiba ni jambo jepesi, bali kuiridhia,” alisema Mbowe.
Alisema katiba ina maeneo mengi yanayohitaji kurekebishwa na kuonya kuwa
iwapo watayafanyia maskhara hawataikubali na watakwenda kuwahamasisha
wananchi ili waungane nao kuikataa.
Mbowe alisema Watanzania hawawezi kuwa na serikali mbili katika mfumo wa
sasa na kupendekeza kuwa Wazanzibari wapewe uhuru wao, ikiwa ni pamoja
na kutekeleza matakwa ya kuwapo pia na serikali ya Tanganyika.
Kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alisema kama CCM wanafikiri
Chadema watakubali kuingia kwenye uchaguzi na tume iliyopo, “basi
wameula wa chuya, hatukubali.”
Alisema kadiri Chadema inavyokua ndivyo maadui nao wanavyozidi kukua,
huku zikitumika mbinu chafu za kuwagawa viongozi na ‘kuwanunua’ wabunge
wake.
Hata hivyo, alionya kuwa hawatasita kuwachukulia hatua za kinidhamu watu
wanaotaka kuwavuruga na kusisitiza kuwa: “Tutakula nao sahani moja.”
No comments:
Post a Comment