JIJI la Dar es Salaam limetajwa kuongoza kwa vifo vingi
vinavyotokana na ajali za barabarani ambazo zinachangia karibu kwa
asilimia 15 ya ajali zote zinazotokea nchini.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga,
alisema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati akielezea
mikakati ya kikosi chake alipozungumza kupitia Televisheni ya Taifa
(TBC).
“Kati ya ajali za nchi nzima 28,531 ambazo ni sawa na asilimia 48 ya
ajali za nchi nzima, lakini hata kwa upande wa vifo utaona Mkoa wa Dar
es Salaam unaongoza kwa kuwa na vifo vingi kwa maana unachangia kwa
karibu asilimia 15 ya ajali zote zinazotokea nchini,” alisema Kamanda
Mpinga.
Kwa upande wa majeruhi alisema kuwa wanaojeruhiwa ni karibu asilimia 37 ya watu wote.
Kwa upande wa ajali za pikipiki mkoani humo alisema tatizo ni kubwa
kwani ajali ni asilimia 48 ya ajali zote huku vifo vikichangia kwa
asilimia 18 na kwa majeruhi wanachangia kwa asilimia 49 ya wote nchini.
Alikiri kwamba pikipiki ni nyingi Dar es Salaam na kueleza kuwa hatua
hiyo imewafanya wajitahidi kutoa mafunzo kwa madereva wa pikipiki kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wa shule za udereva hasa katika mikoa
ya Dar es Salaam, Morogoro na Tanga.
Alisema wanaopata tatizo kubwa ni watembea kwa miguu ambao ndio
wanaokufa zaidi ikilinganishwa na wengine kwani kuanzia Januari hadi
Novemba mwaka jana walifariki dunia 1,118, abiria 1,108, wapanda
pikipiki asilimia 18, baiskeli asilimia 10 , madereva asilimia saba na
wanafunzi ni asilimia tatu.
No comments:
Post a Comment