UTAFITI mpya wa masuala ya uhusiano umebainisha kuwa watu wenye
umri kati ya miaka 35 na 40, ambao hawajaoa au kuolewa wapo kwenye
hatari ya kufa mapema tofauti na waliooa au kuolewa.
Matokeo ya utafiti huo, uliofanywa hivi karibuni
na wataalamu wa masuala ya uhusiano ukiongozwa Dk Ilene Siegler wa Idara
ya Sayansi ya Tabia kutoka Chuo Kikuu kilichopo Kaskazini mwa Jimbo la
Carolina nchini Marekani, umebainisha pia kwamba ndoa ni kinga
inayomwongezea binadamu muda wa kuishi.
Aidha, watafiti hao wamebainisha kwamba wanawake waliopewa talaka au kufiwa na wenza katika umri wa kati wapo kwenye hatari ya kufa mapema zaidi.
Watafiti hao wameeleza kuwa watu ambao maishani
hawajawahi kuoa au kuolewa wapo kwenye hatari ya kufa mapema mara tatu
zaidi ya wale waliokuwa katika ndoa imara katika maisha yao, hasa
wakiwa kwenye umri wa kati.
Matokeo hayo ambayo yalichapishwa kwenye jarida la Annals journal la Marekani na kuandikwa kwenye mtandao wa Daily Mail, ulihusisha watu 4,802, wakiwamo watu waliozaliwa miaka 40 iliyopita.
Ulibaini kuwa kati ya watu wazima wenye umri kama huo wengi wao walikufa wakiwa na miaka 50, kutokana na kuishi peke yao.Kwa kutumia dodoso na maswali ya moja kwa moja
walibaini kuwa pamoja na mtu aliyekuwa kwenye ndoa kuishi kwenye maisha
hatarishi kwa kunywa pombe kupita kiasi na kuvuta sigara, bado walio
kwenye ndoa wana nafasi ya kuishi muda mrefu zaidi kwa asilimia 2.3.
Dk Ilene Siegler, anasema kuwa maisha ya kwenye ndoa ni kinga inayowafanya wanandoa waishi kwa muda mrefu.
“Inaonyesha kuwa na mke au mume ni kinga ya maisha hasa katika umri wa kati, hali hii ikiwaathiri zaidi wanaume, kuliko wanawake,”amesema Siegler.
Alisema kuwa utafiti huo umewawezesha kubaini kuwa
kati ya vifo 238 vilivyotokana na athari za kutokuoa au kuolewa,
wanaume ndiyo waliothirika zaidi na kwamba kati yao wanawake walikuwa ni
32 tu.
Alifafanua kuwa wanaume wameathirika zaidi kutokana na kutokuwa karibu na familia, hivyo kufanya mambo tofauti na mwanamke, ambao hata kama hajaolewa anaweza kuwa karibu na familia na kupata ushauri wa baadhi ya mambo, ingawa hali hiyo haimfanyi kuwa salama,”anasema Siegler.
Dk Siegler alitolea mfano utafiti uliofanywa hivi karibuni na nchi saba za Ulaya akieleza kwamba utafiti huo umeonyesha kuwa mtu aliye kwenye ndoa huwa na furaha kimwili, kiakili na kiafya na humfanya awe na marafiki wazuri, pia hupata ulinzi kwa kuwa wanandoa wana kawaida ya kujilinda wenyewe.
Mtaalamu huyo aliendelea kuutoa ushahidi wa tafiti mbalimbali alizoziona akisema kuwa utafiti kutoka Sweden unaonyesha kuwa wakati ndoa humlinda mhusika dhidi ya maradhi ya Alzheimers, wanaoishi na mpenzi wakiwa kwenye umri wa kati wapo kwenye hatari ya kupata matatizo ya akili.
“Kwa mujibu wa utafiti huo wa Sweden ni kwamba wanawake waliopewa talaka au kufiwa na mwenza kwenye umri wa kati wapo kwenye hatari ya kufa mapema mara tatu zaidi,”anabainisha Siegler.
Matokeo hayo ya utafiti yanaungwa mkono na Dk
Rebeka Sima wa Idara ya Saikolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
akieleza kuwa kwa kawaida, binadamu yeyote ni lazima awe kwenye
uhusiano.
Anasema kwamba kama binadamu hayupo kwenye uhusiano ni lazima atakuwa na upungufu fulani, ambao kibinadamu ni maradhi, ikiwamo msongo wa mawazo na mengine yanayofanana na hayo.
Anasema kwamba kama binadamu hayupo kwenye uhusiano ni lazima atakuwa na upungufu fulani, ambao kibinadamu ni maradhi, ikiwamo msongo wa mawazo na mengine yanayofanana na hayo.
“Hata iweje, wanandoa wanakuwa wanaaminiana kiasi cha kupeana ushauri. Sasa kwa kuwa mpweke ni lazima mhusika atakosa mtu wa kushauriana naye jambo linalosababisha kusononeka na pengine hata kuongea peke yake, kitu ambacho ni hatari zaidi,” anaeleza Dk Sima akiongeza:
“Mpenzi anaweza kuwa wa siku moja au mbili au hata zaidi, lakini uaminifu kati ya mke au mume ni kitu kingine, hivyo walio kwenye uhusiano wa namna hiyo huwa kwenye hatari zaidi kwa kuwa huongeza msongo wa mawazo kutokana na kutokuwa na uaminifu kati ya wahusika.”
Alifafanua kuwa kwa tamaduni za Kiafrika mtu ambaye hajaoa au kuolewa hawezi kutoa ushauri au kuchangia lolote kama walio kwenye ndoa, hivyo mhusika hujitenga mwenyewe kwa kuhisi anadharauliwa, jambo litakalomfanya awe mpweke na kufanya mambo ya kukurupuka.
Naye Modesta Kimonga ambaye ni mtaalamu wa masuala ya saikolojia wa Chuo Kikuu cha Dodoma alisema kuwa binadamu akishakuwa mtu mzima anakuwa na uamuzi binafsi kwa mambo yake na kwamba akiwa na mwenza, mara nyingi hukumbushwa yaliyo mema na kukatazwa mabaya hali ambayo kwa asilimia kubwa husaidia kumfanya mhusika aache mabaya kila anapokumbuka kuwa alikatazwa na mwenza wake.
“Hata kama wanagombana kwa kiasi gani ni lazima
kuna baadhi ya mambo wanashuriana, hasa kwenye matatizo ya kifamilia na
kwenye masuala ya msingi kwa mfano matatizo kazini, ugonjwa na mambo
kama hayo. Hivyo kuna muda ni lazima kwa mtu mzima kuwa na mwenza wake
karibu hii humsaidia sana kupata faraja na kuongeza siku za
kuishi,”amesema Kimonga.
Anasema kuwa kuishi bila mwenza ni hatari zaidi na ndiyo sababu watu wanaoishi hivyo hufa mapema kutokana na kuwa kwenye hatari ya maambukizi ya maradhi hasa ya zinaa na Ukimwi kwa vile huwa huru kujihusisha kwenye uhusiano usio salama.
Godius Kahyarara ambaye ni mhadhiri mwandamizi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha Sayansi ya Uchumi alisema kuwa
kuishi bila kuwa na ndoa kunamfanya mhusika kuweza kujiingiza kwenye
hatari yeye mwenyewe bila kujua ,huku akiamini yupo huru kufanya
chochote na wakati mwingine kuwashangaa waliooa kwa kuwaona wamejifunga.
“Kitu kingine ambacho ni hatari zaidi watu ambao hukaa peke yao iwe wanawake au wanaume hula vyakula visivyo rasmi,hawana muda wa kupumzika na hata uamuzi wao huwa wa kukurupuka na huo ndiyo ugonjwa mbaya zaidi kwani huwasababisha kuwa na afya dhaifu wakiishi maisha hayo kwa muda mrefu afya ambayo ni rahisi kupata maradhi ya kuambukiza kama vile kifua kikuu,magonjwa ya zinaa ikiwemo Ukimwi,”alisema Kahyarara.
Akitoa ushuhuda wake Juma Amrani, ambaye aliwahi kuwa na mke waliyeishi kwa miaka mitatu na kuachana alisema kuwa baada ya kuachana na mke wake huyo hata maisha yake yamebadilika kutokana na kuwa na uamuzi usio sahihi ikiwemo kuuza nyumba waliokuwa wakiishi maeneo ya Boko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na sasa anaishi nyumba ya kupanga huku akikabiliwa na wakati mgumu wa kutokutamani kurudi nyumbani mapema.
“Niko kwenye mipango ya kutafuta mke wa kuoa licha ya kuwa hapo awali niliapa sitafanya hivyo kutokana na vitendo visivyo vya kistaarabu alivyonionyesha mke wangu niliyeachana naye kwa kuwa naona kabisa sipo sawa,” alisema Amrani.
Naye Faidha Abdul ambaye ni mama wa watoto watatu
ambao alizaa bila kuolewa kutokana na kushindwana na wanaume aliozaa
nao, amesema kuwa anapata wakati mgumu sana hasa kwa watoto wa kike
kutokana na matendo yao kuonekana yeye anachangia kwa kuwa na yeye hana
mume.
Alisema kitu hicho kinamkera sana na hutamani angeolewa hata na mwanamume mwingine achilia mbali baba wa watoto hao,ili aweze kuwa angalau na stara.
“Watoto wa kike wamekuwa sasa kwani wameshamaliza
elimu ya Sekondari, kibaya zaidi hawanisikii na walianza uhuni siku
nyingi jambo linalonifanya nikosane na kaka yao akiamini ninafurahia,
huku majirani wakinishutumu kuwa wamefuata tabia yangu ya uhuni kwa kuwa
naishi bila mume. Hali hii inaninyima raha,” alilalamika Faidha.
Kwa upande wake Silvanus Gabriel alisema kuwa alipofiwa na mkewe nusura apoteze maisha kutokana na kukumbwa na maradhi mfululizo ikiwemo kupooza.
Anasema kuwa tatizo lilianza kwa kupungua uzito
bila mpangilio ghafla, baadaye alipata ugonjwa wa kiharusi uliosababisha
mkono na mguu wa kushoto kuishiwa nguvu.
“Nilipokuwa kwenye mazoezi Muhimbili nikakutana na
daktari ambaye nilimfahamu kwa jina moja tu la Dk Thomas, ambapo katika
maongezi ya kawaida alitaka kujua chanzo cha maradhi yangu nikamwambia
sikuwa na tatizo zaidi ya kupungua uzito ambapo nilikuwa na kilo zaidi
ya 80 nikafika kwenye 45 kwa muda mchache ambapo sikuwa na maradhi
yoyote hata homa,” alisema.
Aliongeza: “Akaniuliza tena sikuwahi kupata tatizo siku za nyuma nikamwambia hakuna zaidi ya kufiwa na mke wangu mwaka mmoja uliopita,cha kushangaza dokta alicheka na kuniambia hilo ndiyo tatizo.”
Gabriel amesema kuwa dokta huyo alimshauri kuoa
ambapo yeye mwenyewe alikuwa hataki kwa kuwa watoto wake ni wadogo
akihofiu watapata taabu kulelewa na mama wa kambo lakini alizidi
kumshauri hadi akafikia uamuzi ya kumwoa mwanamke ambaye alikuwa ni
mpenzi wake baada ya kuambiwa kuwa hata kuwa wapenzi mnaokaa mbalimbali
ni tatizo pia kwani kunakuwa hakuna uaminifu.
Gabriel pia aliwashauri wanaume na wanawake
wafuate taratibu ikiwemo kupima afya kabla ya kuoa au kuolewa mapema ili
waweze kuongeza siku za kuishi.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment