KAMPUNI ya mawasiliano ya simu  za mikononi  ya Vodacom Tanzania
 imeingia ubia na shirika la ndege la Fastjet ili wateja wanaosafiri na 
ndege hizo kuweza kulipia tiketi kupitia  huduma ya M-pesa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo jijini Dar es Saaam jana, 
meneja biashara wa Fastjet, Jean Uku, alisema kuwa ubia huo utaongeza 
ufanisi kwa kampuni hizo na wateja kupata unafuu wa kupata tiketi.
Alisema kuwa makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia kampuni hizo 
kutambua umuhimu wa ongezeko la mahitaji ya usafiri katika bara la 
Afrika lenye idadi kubwa ya watu wanaokadiriwa kufikia bilioni moja.
Naye mkuu wa mawasiliano ya bidhaa na huduma za Vodacom, Kelvin 
Twissa, alisema kuwa wanajivunia kuwa suluhisho la mahitaji ya wateja wa
 masoko ya biashara mbalimbali nchini.
  Twissa alisema kuwa kutokana na kuendelea kukua kwa huduma ya M-pesa 
tangu ilipoanzishwa  mwaka 2008, Vodacom inajivunia kuwa wa kwanza 
nchini kuwezesha ulipiaji wa tiketi za mashirika ya ndege kwa njia ya 
haraka.
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment