CHAMA cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Bukoba Mjini, kimeingia katika
siasa chafu za kudhalilishana huku vipeperushi vya kuwatusi madiwani 10
wa chama hicho na wale wa Chama cha Wananchi (CUF) vikisambazwa mitaani.
Madiwani hao waliochafuliwa kwa matusi mazito ya nguoni ambayo mengine
hayaandikiki kwa kuzingatia maadili ni wale nane wa CCM akiwemo Mbunge
wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, na wawili wa CUF waliosaini
hati ya kumtaka mkurugenzi wa manispaa hiyo kuitisha kikao cha dharura
cha Baraza la Madiwani ili kumng’oa Meya Anatory Amani anayekabiliwa na
tuhuma za ufisadi.
Hatua hiyo inakuja siku chache tangu Dk. Amani aamue kupuuza maagizo
ya Makamu Mwenyekiti wao chama hicho taifa, Philip Mangula, kwa kufungua
kesi mahakamani kupinga kujadiliwa na kung’olewa na madiwani.
Mangula ambaye alilazimika kufika mjini Bukoba mwezi uliopita ili
kunusuru mtafaruku huo, aliagiza madiwani nane wa CCM waliokuwa
wamesaini hati hiyo, waondoe tuhuma hizo na kuzipeleka kwenye chama ili
zipatiwe ufumbuzi.
Lakini katika hatua ambayo imetafsiriwa kuwa mgogoro huo unazidi
kushika kasi, juzi vipeperushi hivyo vya matusi vilisambazwa na watu
wasiojulikana kwa kuvibandika katika maeneo mbalimbali ya mji wa Bukoba.
Madiwani waliosaini hati ya kutaka kuitishwa kikao cha kumng’oa meya
huyo mbali na Kagasheki ni Naibu wake, Alexander Ngalinda (Kata ya
Buhende) na Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM
Manispaa ya Bukoba.
Wengine ni Richard Gasper (Miembeni), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo),
Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe) na Mulubi
Kichwabuta (Viti Maalumu) na wale wa CUF ni Ibrahim Mabruk (Bilele) na
Rabia Badru wa Viti Maalum.
Taarifa kutoka mjini Bukoba zilisema kuwa madiwani hao nane wa CCM,
jana waliandika barua ya malalamiko kwenda kwa katibu wa chama hicho
wilaya na nakala zake kwa mwenyekiti wa mkoa, mkuu wa mkoa na Mangula.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, barua hiyo ambayo ilikabidhiwa asubuhi
wamekataa kushiriki vikao vyovyote vitakavyoongozwa na Meya Amani
wakimtuhumu kuwa ndiye alihusika kusambaza vipeperushi hivyo vya
kuwakashfu.
“Na katika kutimiza msimamo wetu, tayari madiwani wote nane wa CCM leo
tumesusia kikao cha meya kilichojadili maandanlizi ya Baraza la
Madiwani.
“Na kwa mujibu wa kanuni baada ya kukataa idadi ilikuwa haimruhusu
kwendelea na kikao kwani wajumbe tuko 17 lakini alibaki na saba ambao ni
pungufu,” alisema mmoja wa madiwani hao.
Katika vipeperushi hivyo, madiwani hao kila mmoja ametajwa kwa jina
lake, kata na orodha ya tuhuma zake huku wengine wakidaiwa kulaghaiwa
kwa fedha na mmoja wa viti maalum akidhalilishwa kwa tuhuma za ngono.
Mgogoro wa Bukoba mjini umekuwa na muda mrefu sasa na Meya Amani
katika kujihami ili asing’olewe, kwa kushirikiana na mkurugenzi wake,
Hamis Kaputa, walilazimika kuahirisha kikao cha Baraza la Madiwani
kinyume na kanuni.
Kwa mujibu wa sheria namba 8 ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982
kifungu namba 7 (1), mkurugenzi anapaswa kumwandikia barua kila mjumbe
kumweleza mahali na siku vikao vitapofanyika na ajenda zitakazojadiliwa
siku saba kabla ya kikao.
Madiwani hao hawakuwahi kujulishwa uwepo wa kikao hicho
walichotaarifiwa na mkurugenzi kuwa kimesogezwa mbele kama kanuni hizo
zinavyosema.
Kikao hicho kilikuwa cha kujadili utekelezaji wa shughuli za robo
mwaka za fedha kati ya Oktoba hadi Desemba 30 mwaka jana, na kwa mujibu
wa sheria kilipaswa kufanyika si zaidi ya Januari mwaka huu.
Katika barua hiyo yenye kumb. Na BMC/C.50/5/13, inayosomeka ‘Yah:
Kusogezwa mbele ratiba ya vikao vya Baraza la Madiwani’, Kaputa hata
hivyo haonyeshi ni lini kikao hicho kitakaa.
Kaputa, katika barua hiyo anadai kuwa baraza haliwezi kufanyika
kutokana na wakuu wa idara wengi kuwa safarini kuelekea jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya vikao vya bajeti 2013/2014.
Amani ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kagondo, aliamua kwenda mbali
zaidi huku akikiuka kanuni na sheria ambapo sasa amefungua pingamizi
mahakamani ili kuzuia mkurugenzi asiitishe kikao chochote cha kujadili
tuhuma zake kwa muda wote atakaokuwa katika wadhifa wake.VIA TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment