KWA mara nyingine tena Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), kimekiliza Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya Mbunge wake wa
Meatu, Meshack Opurukwa, kushinda kesi katika Mahakama ya Rufaa ya
Tanzania, kwa pingamizi la awali kutokana na mlalamikaji kutofuata
sheria katika kukata rufaa.
Kesi hiyo iliyokuwa imefunguliwa na mpiga kura wa jimbo hilo, ambaye
pia ni Katibu wa Mbunge aliyeshindwa, Masanja Salu, ilitupiliwa mbali na
jopo la majaji, Edward Rutakangwa, Catherine Urio na Mbarouk Salum
Mbarouk.
Katika kesi hiyo, mlalamikaji Salu, alikuwa na madai matatu tangu
awali, la kwanza likiwa ni kutumia ukabila kwenye kampeni, tofauti ya
kura zilizotangazwa na msimamizi wa uchaguzi na zile zilizopelekwa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi na mlalamikaji kudai kuwa Opurukwa alikiuka
taratibu za kampeni kwa kujiendea bila utaratibu.
Awali katika kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa katika Mahakama Kuu
Kanda ya Tabora, mbele ya Jaji Fredrick Wambali, mlalamikaji alishindwa
kuthibitisha malalamiko yake, hivyo mahakama hiyo kumpa ushindi
Opurukwa Mei 4 mwaka jana.
Kufuatia ushindi huo, mlalamikaji hakukubali na hivyo alikata rufaa,
lakini jana mahakama iliitupitia kwa kuwa mlalamikaji aliikata nje ya
muda.
Kesi hiyo ambayo upande wa mlalamikaji uliwakilishwa na wakili Jackson
Brashi, huku Opurukwa akiwakilishwa na Godwin Muganyizi imefutwa kwa
kuwa haikufuata sheria (null ab initio).
Desemba 21 mwaka jana, Mahakama ya Rufaa, nchini katika kesi za
uchaguzi ilitoa mwongozo kuwa ‘mpiga kura hana haki ya kisheria kufungua
kesi kuhoji matokeo ya uchaguzi pale ambapo haki zake hazikukiukwa’.
Mahakama iliongeza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya
Tanzania, raia anakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi kwa maslahi ya
jamii, kama ilivyotokea katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila
dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya mwaka 1995.
Ilisema kesi dhidi ya wagombea wakitolea mfano kesi ya Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), aliyeshtakiwa na wapiga kura
hazikufunguliwa chini ya Ibara ya 26 (2) ambayo inampa fursa na haki
raia yeyote kufungua shauri mahakamani lenye masilahi ya umma.
No comments:
Post a Comment