MATOKEO mabaya ya mtihani wa kidato cha nne yamezidi kuibua
mapya, baada ya wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini kusema mitihani
ilitungwa kwa mfumo tofauti na uliozoeleka miaka yote, huku tume
iliyounndwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ikipondwa na baadhi ya watu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo
Binafsi nchini (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema kwamba maswali
waliyoulizwa watahiniwa yalikuwa ya kujieleza tofauti na miaka ya nyuma,
ambapo mfumo uliotumika uliwataka watahiniwa kutaja vitu tu bila ya
kulazimika kuvielezea kwa undani.
Kauli yake iliungwa mkono na Mkuu wa Taaluma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian, Florence Mapunda ambaye alisema kuwa mtihani wa mwaka jana ulitaka zaidi watoto kujieleza tofauti na miaka ya nyuma wakati wanafunzi walipokuwa wanakariri.
Hata hivyo, Msemaji wa Baraza la Mitihani Tanzania
(Necta), John Nchimbi alisema mfumo wa mtihani haukubadilika kwa namna
yoyote na kuwa upo kama ule wa miaka yote.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip
Mulugo, kwa upande wake alisema madai yanayotolewa hayana msingi, huku
akihoji kwa nini yasitoke tangu mitihani ilipokuwa ikifanyika na badala
yake yanatoka baada ya kutangazwa kwa matokeo.
Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne.
Kutokana na matokeo hayo, Waziri Mkuu Pinda, juzi
alitangaza kuunda tume ya kuchunguza chanzo cha matokeo hayo kuwa
mabaya, hatua ambayo hata hivyo imekosolewa na wasomi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM).
Tume hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka Taasisi za
Elimu, Chama cha Waalimu, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa
Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa) inatarajiwa kuanza kazi
wiki hii.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuunda tume ni kupoteza muda kwa sababu matatizo na changamoto zote ndani ya sekta hiyo yanajulikana, huku mwenzake, Profesa Chriss Maina pia wa UDSM akisema kuunda tume hakutaisaidia kwa kuwa Serikali inaidharau sekta ya elimu.
“Tatizo ni kutowekeza kikamilifu katika sekta ya elimu, imekuwa na matumizi makubwa katika mambo yasiyokuwa ya lazima,”alisema Profesa Mpangala.
Alisema matatizo mengine ni mazingira magumu ya
kufundisha na uhaba wa walimu. “Kinachotakiwa wajipange kufanyia kazi
changamoto hizi zilizopo badala ya kuunda tume, wakati fedha nyingi
tunasikia inapotea kwenye ubadhirifu,”alisema Profesa Mpangala.
Naye Profesa Maina alisema: “Hiyo tume ya kazi
gani kwa sababu matatizo yanafahamika wazi, umewahi kusikia taifa gani
ambalo halina mtalaa wa elimu. Hiyo ndiyo hali halisi kwa nchi yetu. ”
Kauli ya TAMONGSCO
Mringo alisema mfumo huo umetokana na mtalaa mpya ambao unataka zaidi kuangalia uwezo tofauti na ule wa nyuma ambao uliwafanya wanafunzi wawe wanakariri zaidi, lakini akakosoa utaratibu wa kuanza kutumika kwake bila watahiniwa kufundishwa.
Mringo alizitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na wizi na udanganyifu wa mtihani ulidhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Msemaji wa Necta, Nchimbi alisema mfumo wa mitihani ulibadilika 2008 baada ya mtalaa kubadilika kwa kuondoa baadhi ya mada za masomo na kuweka mpya.
Kauli ya TAMONGSCO
Mwenyekiti wa TAMONGSCO, Mringo alisema: “Kwenye
mitihani ya miaka ya nyuma, mtu alikuwa anaulizwa kwa mfano, taja sehemu
tatu za mti. Akitaja mizizi, shina na matawi anakuwa amepata.”
Aliongeza: “Mwaka jana mtihani ulivyokuwa ni
kwamba walikuwa wanatakiwa kutaja sehemu tatu za mti, halafu wanaambiwa
waseme ni nini kinazunguka mti huo. Hapo ndiyo ilifanya mambo kuwa
magumu.”
Mringo alisema mfumo huo umetokana na mtalaa mpya ambao unataka zaidi kuangalia uwezo tofauti na ule wa nyuma ambao uliwafanya wanafunzi wawe wanakariri zaidi, lakini akakosoa utaratibu wa kuanza kutumika kwake bila watahiniwa kufundishwa.
Kwa mujibu wa Mringo, ili watoto waweze kujibu aina hiyo ya maswali, inatakiwa waandaliwe kuanzia kwenye shule za msingi.
Alisema pia kuwa, mwaka huu alama za maendeleo ya
mwanafunzi katika mitihani ya shule (continuous assessment) hazikutumika
kama miaka mingine ambayo alama hizo zilikuwa zikichangia kwa asilimia
40 katika mtihani wa mwisho.
Mringo alizitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na wizi na udanganyifu wa mtihani ulidhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Naye Mapunda alisema:“ Mtihani wa mwaka jana
ulikuwa unapima zaidi uwezo wa watoto kuelewa siyo kukariri. Miaka ya
nyuma watoto walikuwa wanaogopa zaidi mitihani ya ndani ya shule kuliko
ile ya nje, ukiwaambia wasome kwa ajili ya mtihani wa taifa wanasema
haina shida siyo migumu na kuwa ile ya ndani ndiyo ilikuwa migumu
zaidi.”
Necta na Mulugo
Msemaji wa Necta, Nchimbi alisema mfumo wa mitihani ulibadilika 2008 baada ya mtalaa kubadilika kwa kuondoa baadhi ya mada za masomo na kuweka mpya.
“Tangu 2008, mitalaa ya fizikia na kemia tu ndiyo
haikubadilika, yenyewe ilikuja kubadilika 2011 na katika kipindi chote
mitihani imekuwa ikitungwa kwa mfumo huo huo na hakuna watu
waliolalamika,” aliongeza Nchimbi.
Naye Mulugo alisema kwa sasa watu wanatoa sababu
nyingi na kuhadharisha kuwa ni vizuri wakaiachia tume iliyoundwa na
Waziri Mkuu ifanye kazi yake.
Mulugo alisema Necta ni chombo cha kusimamia mitihani, lakini
mitihani inatungwa na walimu pamoja na maofisa elimu na kusahihishwa na
walimu wenyewe.
“Kwa nini haya madai wayatoe sasa hivi, sababu za
msingi ninazoziona mimi ni kuwa watoto sasa hivi hawasomi, hebu tuache
tume iliyoundwa ifanye kazi yake kwa sababu itaangalia ngazi zote za
mitihani,”alieleza Mulugo.
No comments:
Post a Comment