KAMA ni mtoto, unaweza kusema si riziki. Hivi ndivyo hali
ilivyo ndani ya klabu ya Simba, ambako imeendelea na mwenendo wa shaka
katika Ligi Kuu Tanzania bara, baada ya jana kukubali kichapo cha bao
1-0 kutoka kwa wakata miwa wa Mtibwa Sugar kwenye dimba la Taifa jijini
Dar es Salaam.
Simba ambao ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo, msimu huu imekuwa na
mwenendo mbovu na hata kufuta mawazo ya kutetea taji hilo miongoni mwa
mashabiki wake, ambao hivi sasa wako katika hali mbaya kutokana na
kufanya vibaya.
Hadi sasa, Simba imepoteza mechi tatu huku ikijikongoja katika nafasi
ya tatu ikiwa na pointi 31 baada ya kushuka dimbani mara 18. Yanga
wako kileleni kwa pointi 39 huku Azam ikifuatia kwa pointi 36.
Katika mechi ya jana, Simba ilianza kwa kasi na dakika ya tatu tu,
Shomari Kapombe alipokea pande la Amir Maftah, lakini shuti lake
likaokolewa na kipa Hussein Sharrif, kabla ya Mtibwa kujibu
mashambulizi na kupata kona ambayo haikuzaa matunda.
Alikuwa ni Salvatory Ntebe dakika ya 16, aliyeiandikia Mtibwa bao
hilo la pekee, baada ya kuunganisha mpira uliotokana na kona.
Dakika ya 41, Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na nafasi yake kuchukuliwa na Kigi Makasi.
Redondo baada ya kutoka alikwenda moja kwa moja kwenye vyumba vya
kuvalia badala ya benchi la wachezaji wa akiba. Kitendo kama hicho
kilifanywa na Haruna Moshi ‘Boban’ siku walipocheza na Libolo kwenye
uwanja huo.
Hadi mwamuzi Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga akiashiria mapumziko, Mtibwa walikuwa mbele kwa bao hilo.
Kipindi cha pili, Simba walirejea kwa nguvu na dakika ya 49, shuti la
Haruna Chanongo lilipaa langoni mwa Mtibwa sentimita chache.
Simba walifanya mabadiliko tena dakika ya 51, kwa kumtoa Boban na
nafasi yake kuchukuliwa na Amri Kiemba, ambako kabla ya kutoka,
alimkumbatia Kigi Makasi na kama mazoea yake, alikwenda moja kwa moja
vyumbani.
Dakika ya 86, Simba ilipata pigo, baada ya Juma Nyoso kulimwa kadi
nyekundu kutokana na kumkwatua Vicent Barnabas wakati mpira ukiwa
umetoka nje. Hadi Mwamuzi Kidiwa akimaliza mpira, Mtibwa iliibuka
kidedea kwa bao 1-0.
Matokeo hayo yaliibua vurugu miongoni mwa mashabiki wa Simba, ambao
walitaka kuvamia jukwaa kuu kuwashughulikia baadhi ya viongozi
waliokuwepo.
Kutokana na hali hiyo, polisi iliwalazimu kufunga baadhi ya njia za
kuingilia maeneo ya jukwaa kuu ili kuwanusuru viongozi hao, hali ambayo
ilisababisha adha kubwa kwa mashabiki wakati wa kutoka.
Lakini mashabiki hao wa Simba, walibaki nje ya uwanja wakiwa katika
vikundi vikundi, hali iliyosababisha wachezaji kufungiwa vyumbani.
Mashabiki hao walisikika wakiutupia lawama uongozi huku wakidai
hawamtaki kocha, Mfaransa Patric Liewig.
Hali ilizidi kuwa mbaya, ambako Uwanja wa Taifa uligeuka uwanja wa
vita, baada ya polisi kulazimika kutumia maji ya kuwasha kuwatawanya
mashabiki hao, huku basi la Simba likiondoka likisindikizwa kwa ulinzi
wa hali ya juu.
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Masoud ‘Cholo’, Amir Maftah, Juma Nyoso,
Komanbil Keita, Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna
Moshi ‘Boban’/Amri Kiemba, Haruna Chanongo/Mrisho Ngasa, Ramadhani
Chombo ‘Redondo’/Kigi Makasi.
Mtibwa: Hussein Sharrif, Said Mkopi, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’,
Salvatory Ntebe, Salum Swedi, Shabani Nditi, Jamal Mnyate, Hussein
Javu/Juma Liuzio, Shabani Kisiga ‘Malone’, Rashid Gumbo, Vicent
Barnabas.
No comments:
Post a Comment