KOCHA wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema haoni
sababu za kikosi chake kushindwa kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika
zitakazofanyika 2015 nchini Morocco.
Mara ya mwisho Taifa Stars ilifuzu kushiriki Fainali za Afrika miaka 33 iliyopita nchini Nigeria na Taifa Stars kutolewa katika hatua ya makundi.
Ni wazi mwisho wa fainali hizi za 2013 utakuwa mwanzo wa fainali nyingine za 2015, ambapo ili kuweza kushiriki fainali za 2015 inabidi kufanya vizuri katika hatua ya makundi ya kufuzu kushiriki fainali hizo.
Mara kwa mara tumeshuhudia timu inayoshika nafasi ya kwanza katika kila kundi katika mashindano ya kuwania kufuzu ndiyo hufuzu kushiriki fainali, hivyo kuna umuhimu wa kuchagua wachezaji wenye uwezo.
Tunaungana na Kocha Poulsen kuamini Taifa Stars ina kila sababu ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika 2015, lakini hilo litawezekana iwapo maandalizi mazuri yatafanyika.
Taifa Stars inaweza kufuzu kama wachezaji wanaochaguliwa kikosi hicho watakuwa na uzalendo wa hali ya juu, umoja na kuwa na lengo moja, kwa sababu lengo moja huleta ushindi.
Tunasema hivyo kwa sababu tunafahamu wachezaji wa timu ya Taifa kazi yao kubwa ni kupigania kitu ambacho huwa na thamani na kumbukumbu kubwa kwa vizazi vingi vitakavyofuatia.
Kitu wanacholeta wachezaji wa timu ya Taifa ni ushindi, siku zote wachezaji wanaposhinda huwa wanaliletea Taifa lao furaha na kujisikia fahari kuishi katika taifa hilo.
Wachezaji hawatakiwi kuwa wabinafsi wanapokuwa uwanjani ila wanatakiwa kucheza kitimu na kusaidiana ili kulipigania taifa lao kwa hali.
Wanatakiwa pia kutambua umuhimu na wajibu wanaokuwa nao wakati wakiliwakilisha taifa, pia wafahamu hiyo ndiyo nafasi yao kujitangaza.
Tunarudia tena kusema kuwa, tunaungana na
Kocha Poulsen kwamba tunaweza kufuzu kushiriki Fainali za Afrika 2015
kwani timu ya Cape Verde iliweza kufuzu na kushiriki Fainali za Afrika
2013 kwa mara ya kwanza wakati katika Fainali za Afrika 2012 timu za
Niger na Botswana zilifuzu kwa mara ya kwanza pia.
Nchi za Botswana na Niger hazikufuzu kirahisi kushiriki katika fainali hizo za Afrika 2012, ila zilipambana katika makundi yao na kuzishinda timu kubwa kama Misri, Afrika Kusini na Tunisia na kushika nafasi ya kwanza katika makundi yao.
Pia Cape Verde haikufuzu kirahisi Fainali za Afrika 2013 kwani ilizifunga Madagascar na Cameroon na kukata tiketi ya kushiriki fainali hizo za Afrika.
Tanzania inatakiwa kufanya kama zilivyofanya Botswana, Niger na Cape Verde ili kuhakikisha inafuzu kushiriki fainali za Afrika zijazo, lakini ni wazi inatakiwa kuhakikisha inamaliza ya kwanza katika kundi wakati wa mechi za kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Afrika.
Ili kufanikisha hilo inabidi tuwe na wachezaji mahiri katika safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji, pia viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanatakiwa kuwa na mipango sahihi ya kuhakikisha tunafuzu kushiriki fainali za Afrika.
Hatutaweza kufuzu kama hatuna nia ya dhati ya kutaka kufuzu na kushiriki fainali hizo, ambapo tunatakiwa tuandae wachezaji wenye vipaji wanaoweza kushindana katika kiwango cha juu, wenye akili ya mchezo, mwili, stamina na kasi.
No comments:
Post a Comment