MTU
mmoja, Omar Mussa Makame (35), mkazi wa Mwanakwerekwe Zanzibar,
amekamatwa na Jeshi la Polisi Zanzibar, kwa tuhuma za mauaji ya
aliyekuwa Padri wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Evaristus Mushi. Taarifa
hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Kamishna wa Jeshi hilo Zanzibar, Mussa
Ali Mussa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Kamishna Mussa, mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 13, mwaka huu, katika Mtaa wa Kariakoo, Zanzibar na atafikishwa mahakamani baada ya taratibu zote kukamilika.
“Huu ni mwanzo tu, kwani Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi wa kitaalamu ili kuhakikisha watu wote wanaohusika na matukio ya uhalifu hapa Zanzibar, wanakamatwa na kufikishwa katika mkondo wa sheria.
“Jalada la mtuhumiwa huyu tayari limeshapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria kwa sababu yeye ndiye atakayetupa mwongozo juu ya suala hili.
“Kabla mtuhumiwa hajakamatwa, tulifanya upelelezi kwa kutumia michoro na alipokamatwa, watu waliokuwa eneo la tukio siku ambayo padri aliuawa, walimtambua kwamba ndiye aliyekuwapo.
“Pamoja na kazi nzuri tunayoifanya kwa kushirikiana na wananchi, bado tunahitaji msaada wao katika harakati zetu za kukabiliana na uhalifu,” alisema Kamishna Mussa.
Padri Mushi aliuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi kichwani Februari mwaka huu, wakati akiingia katika Kanisa Katoliki, Kigango cha Mtakatifu Theresia, Zanzibar.
Baada ya watu hao kufanya mauaji hayo, walitoweka kwa kutumia pikipiki waliyokuwanayo wakati wanamsubiri padri huyo awasili kanisani hapo.
Kutokana na uzito wa tukio hilo, Jeshi la Polisi nchini, lilifanya upelelezi kwa kuwashirikisha wataalamu wa masuala ya upelelezi kutoka Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ambao waliwasili Kisiwani Zanzibar na kuchora michoro kuonyesha jinsi mauaji hayo yalivyofanyika.
Juzi, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuonyesha jinsi asivyoridhishwa na ukimya wa upelelezi wa kuuawa Padri Mushi na kujeruhiwa kwa risasi, Padri Ambrose Mkenda.
No comments:
Post a Comment