JESHI la Polisi Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi linawashikilia
watu wawili wakazi wa Kijiji cha Igalila Kata ya Mpanda Ndogo, Tarafa
ya Kabungu kwa tuhuma za kumuua mwenzao, Rehani Pesambili (70), kwa
kumpiga mateke na ngumi wakati wakinywa pombe ya kienyeji aina ya
komoni.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Emmanuel Nley, aliwataja
watuhumiwa hao kuwa ni Geofrey Pesambili (24) na Efram Adamu ( 28) .
Alisema tukio hilo lilitokea Aprili 20, mwaka huu majira ya saa
5:00 usiku wakati marehemu akinywa pombe hiyo pamoja na watuhumiwa
hao nyumbani kwa Jumanne Jailos.
Alisema wakiwa eneo hilo marehemu aliwaambia wenzake kuwa kofia
yake imeibiwa akiwa hapo ndipo watu hao walipowahisi watoto wa
Jumanne waliokuwa wakiwauzia pombe hiyo kuichukua, hivyo kuanza
kuwachapa viboko lakini kofia hiyo haikuweza kupatikana.
Kamanda Nley alisema baadaye watuhumiwa hao waliamua kumpekua
marehemu ili kutaka kupata ukweli kwamba kofia hiyo anayo au la, na
baadaye kuikuta ikiwa ndani ya suruali yake na walipomuuliza aliwajibu
kuwa alikuwa amesahau kama alikuwa ameiweka mfukoni mwake.
Baada ya kuona hivyo watuhumiwa hao walitaka marehemu naye
aadhibiwe kwa kuchapwa viboko kwa kuwa aliwasababishia watoto hao
kuchapwa viboko kwa kosa ambalo halikuwa lao.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, wakati watuhumiwa hao wakimchapa
marehemu viboko visivyo na idadi aliamua kujihami kwa kuchukua kigoda
na kuwarushia, hali iliyosababisha amjeruhi Jumanne.
Alisema tukio hilo liliwafanya wapate hasira ndipo nao
walimshambulia marehemu kwa mateke na ngumi, hali iliyomfanya apate
maumivu kisha aliondoka na kurudi nyumbani kwake na siku iliyofuata
alifariki dunia akiwa nyumbani hapo majira ya mchana.
Kamanda Nley alisema watuhumiwa watafikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi utakapokamilika.
No comments:
Post a Comment