MBUNGE wa Viti Maalumu, Dk. Pudenciana Kikwembe (CCM) ameeleza
kukerwa na majibu ya Naibu Waziri wa Elimu na Ufundi, Philipo Mulugo
yasiyotoa majibu ya kina kuhusu walimu kukatwa asilimia mbili ya
mshahara.
Kikwembe alitoa kauli hiyo bungeni jana alipouliza swali la nyongeza
kwa kuitaka serikali ieleze ni kwa sababu gani walimu wamekuwa wakikatwa
fedha hizo bila kushirikishwa.
“Mheshimiwa spika napenda kusema nasikitishwa na majibu ya naibu
waziri kwa kushindwa kutoa majibu ambayo ni ya uhakika, si kweli kuwa
walimu wanaokatwa asilimia mbili ya mshahara wao wanakuwa
wameshirikishwa, hata mimi nilikuwa mwalimu, nilikuwa nikikatwa, lakini
sijawahi kushirikishwa,” alisema Dk. Kikwembe.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alisema walimu wanakatwa asilimia
mbili ya mishahara kwa ajili ya kuchangia Chama cha Walimu Tanzania
(CWT), lakini wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu.
Kutokana na hali hiyo, alihoji ni kwanini chama hicho hakioni umuhimu
wa kuwapatia walimu mikopo isiyokuwa na riba kama vile ujenzi wa nyumba,
ili kuwakwamua katika mazingira magumu ya kimaisha.
Akitolea ufafanuzi wa swali la nyongeza la Dk. Kikwembe, Waziri wa
Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka alisema kwa sasa ametoa agizo kwa
waajiri kutowakata asilimia mbili ya mishahara walimu ambao ni ajira
mpya hadi hapo watakapopatiwa elimu juu ya makato hayo.
Kwa upande wake, Mulugo akijibu swali la msingi alisema kwa sasa CWT
kipo kwenye hatua za mwisho za kufungua Benki ya Walimu ambayo itaanza
kufanya kazi Juni mwaka huu.
Alisema benki hiyo itakapoanza kila mwalimu atakuwa na haki ya kukopa
kwa ajili ya mahitaji yake kama vile kujenga nyumba, kusomesha, watoto
wao ama kujisomesha wao wenyewe.
No comments:
Post a Comment