Rais wa zamani wa Madagascar, Mark Ravalomanana ametangaza kuwa,
mke wake Lalao Ravalomanana atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Julai 24.
Lalao ni mwanamke wa 4 kujitosa uwanjani na anatarajiwa kuchuana na
vigogo wengine wa kisiasa nchini humo.
Rais wa sasa Andry Rajoelina
aliingia madarakani mwezi Machi mwaka 2009 baada ya kumpindua Mark
Ravalomanana. Baada ya hapo, kiongozi huyo aliyepinduliwa alikimbilia
uhamishoni Afrika Kusini.
Duru za habari zinaarifu kuwa, uamuzi wa Mark Ravalomanana wa
kumpendekeza mke wake kuwania urais, umepata baraka kutoka kwa wapambe
wake wa karibu. Hii ni katika hali ambayo, uchunguzi wa maoni uliofanywa
hivi karibuni nchini Madagascar unaonyesha kuwa, watu wengi
wanapendelea nchi iongozwe na rais mwanamke.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, makubaliano ya kutatua hali ya kisiasa
ya Madagascar yanamzuia Andry Rajoelina na Mark Ravalomanana kuwania
urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.
No comments:
Post a Comment