MWALIMU wa Shule ya Msingi Msoga, Joel Mjema anatuhumiwa kuwatia mimba wanafunzi wawili wa msingi na sekondari.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, Ahmed Kipozi alisema
mwanafunzi mmoja anasoma darasa la sita Shule ya Msingi Msoga na
mwingine anasoma kidato cha tatu Shule ya Sekondari Msoga.
Kipozi alimuagiza Mkuu wa Kituo cha Polisi Chalinze kuhakikisha mwalimu huyo anatiwa mbaroni haraka.
Aidha, Mkuu huyo amekemea tabia ya wazazi kushawishika na fedha ili
kumaliza kesi zinazohusu watoto wao kutiwa mimba na walimu.
Aliwataka wanafunzi kutoshiriki mapenzi na walimu wao wangali shuleni kwani kwa kiasi kikubwa wanarudisha nyuma maendeleo yao.
Wakati huo huo, watu watatu wa jamii ya Kimasai wanaotuhumiwa kuwabaka wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ubena wanatafutwa.
Kipozi alisema watu hao wanaofanya kazi ya uchungaji mifugo ambao
majina yao yamehifadhiwa kwa taratibu za upelelezi, wanasadikiwa kufanya
vitendo hivyo mara kwa mara na kuwatia hofu wanafunzi wanaosoma katika
shule hiyo ya kutwa.
Alimuagiza Mkuu wa Kituo cha Polisi Chalinze kuhakikisha anawatia
mbaroni watuhumiwa hao baada ya taarifa zao kufikishwa kwake.
Alisema ikishindikana washikwe waajiri wao hadi hapo watuhumiwa hao
watakapokuwa wamepatikana ili waweze kufikishwa katika mikono ya dola.
Imebainishwa kuwa wachungaji hao wamejenga tabia ya kuwavizia
wanafunzi wasichana katika vichaka vilivyopo katika njia inayoelekea
shuleni hali ambayo imesababisha wanafunzi wa kike kuhofia usalama wao
pindi wanapokwenda na kurudi shule.
No comments:
Post a Comment