MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA)
imetangaza nauli mpya kwa usafiri wa barabarani, reli pamoja na
kupandisha tozo mbalimbali za kuhudumia meli bandarini.
Akitangaza nauli hizo mpya ofisini kwake jana ambazo zitaanza kutumika
rasmi Aprili 12 mwaka huu, Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmad Kilima
alisema kwa upande wa usafiri wa barabarani mamlaka baada ya kupitia
maombi mbalimbali ya wadau imeamua kuongeza kiwango cha nauli kwa
wastani wa asilimia 24.46 kwa daladala badala ya asilimia 149
zilizopendekezwa.
Wakati kwa mabasi ya masafa marefu, viwango vimeongezwa kwa asilimia
20.3 kwa mabasi ya kawaida, asilimia 16.9 kwa mabasi daraja la kati na
asilimia 13.2 kwa mabasi ya daraja la juu badala ya nyongeza kati ya
asilimia 35 na asilimia 48.5 iliyoombwa awali na wadau hao.
Kwa upande wa daladala jijini Dar es Salaam, Kilima alisema kuanzia
kilometa 0-10 (sawa na
Ubungo–Kivukoni) itakuwa sh 400, huku kilometa
kati ya 11-15 (sawa na Mwenge–Temeke) itakuwa ni sh 450 na kwa umbali wa
kilometa inayoanzia 16-20 (sawa na Tabata Chang’ombe–Kivukoni) itakuwa
sh 500.
Umbali wa kilometa 21-25 (swa na Pugu Kajiungeni-Kariakoo) itakuwa sh
600 na umbali wa kilometa 26-30 (sawa na Kibamba-Kariakoo) itakuwa ni
sh 750.
Alisema kwa upande wa wanafunzi itakuwa ni sh 200 ambayo ni nusu ya
nauli ya mtu mzima ya kiwango cha chini cha nauli ya sh 400, na nauli
hiyo itatumika kwa njia zote za Jiji la Dar es Salaam.
Kwa upande wa mabasi ya masafa marefu alisema basi la kawaida kwa njia
ya lami itakuwa sh 30,700 kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya, basi la
hadhi ya kati (semi luxury) sh 61,400 ambapo itakuwa ni kutoka Dar es
Salaam hadi Mwanza na sh 36,000 kwa basi la hadhi ya juu (luxury) ambapo
itakuwa ni kutoka Dar es Salaam hadi Arusha.
“Ili kutoa huduma zinazokidhi viwango vipya vya nauli tumetoa maagizo
kwa wamiliki wa mabasi haya kutotumia wapiga debe katika kuuza tiketi,
kufuata kanuni za Sumatra za udhibiti wa tozo za nauli ambazo zinahimiza
kuwepo kwa kumbukumbu sahihi za mahesabu ili kurahisisha mapitio ya
viwango vya nauli.
Kwa usafiri wa reli, Kilima alisema baada ya mchakato wa kupitia
mapendekezo ya watoa huduma kukamilika, mamlaka iliridhia viwango vipya
vya nauli kwa madaraja yote ambapo iliamua kuongeza viwango vya juu vya
daraja la kwanza na la pili kwa wastani wa asilimia 25 na daraja la tatu
kwa asilimia 44.1.
Alisema kwa sasa nauli kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kwa daraja
la kwanza itakuwa sh 21,100 ambapo awali ilikuwa sh 16,852; Dar es
Salaam- Dodoma (sh 34,700), Dar es Salaam-Tabora (sh 54,800), Dar es
Salaam-Mwanza (sh 74,800), Dar es Salaam-Kigoma (sh 60,599) na Dar es
Salaam-Shinyanga sh 65,300.
Kuhusu tozo mbalimbali katika kuhudumia meli katika bandari
zinazomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Kilima alisema
Mei mwaka 2012, TPA iliwasilisha mapendekezo kwa Sumatra ili kufanya
mapitio mbalimbali ya gharama za bandari.
Alizitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na tozo za nahodha kuingiza meli
(Pilotage Fees), huduma za kufunga meli gatini, uondoshaji taka melini,
tozo ya meli inayosubiri kazi au maelekezo na gharama za leseni na ada.
Nyingine ni tozo ya kuhudumia meli za mafuta.
Gharama za huduma zipatazo 19 zilifanyiwa mapitio na viwango vipya kuridhiwa. Gharama hizi hulipwa na wenye meli.
“Kwa mujibu wa maombi hayo, TPA walipendekeza tozo hizo kuongezeka kwa
kati ya asilimia 7 hadi 400 kulingana na aina ya huduma zinazotolewa
kwa meli zinazotumia bandari zinazomilikiwa na TPA.
Hata hivyo mamlaka imeridhia ongezeko la gharama kwa wastani wa
asilimia 34.3. Gharama zilizofanyiwa mapitio kwa mara ya mwisho mwaka
1994 kabla ya hazijapitiwa tena mwaka huu,” alisema Kilima.
Alisema kwa sasa tozo mpya kwa nahodha kuingiza meli ni dola 150, tozo
ya bandari dola 13.40, tozo ya kuongoza ni dola 6, tozo ya kuegesha
meli ni dola 0.50 na tozo ya huduma ya tagi ni dola 20.
Katika kipindi cha fedha cha 2011/2012, Sumatra ilipokea maombi rasmi
kutoka kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa barabara zikiwemo kampuni
za usafirishaji abiria zikipendekeza mapitio ya viwango vya nauli za
mabasi yanayotoa huduma za usafiri mijini (daladala) na yanayotoa huduma
katika mikoa kufuatia ongezeko la gharama za uendeshaji kwa mujibu wa
mawasilisho yao.
No comments:
Post a Comment