MWALIMU wa shule ya msingi iliyopo maeneo ya Machori, Yohana
Burugu, ameifikisha Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mahakamani na kudai
zaidi ya sh milioni sita na kurejeshwa kazini bila masharti baada ya
kuondolewa katika ajira kinyemela.
Kwa mujibu wa hati ya kuitwa katika Mahakama ya Kazi na Usuluhishi
Musoma, halmashauri hiyo imetakiwa kufika katika mahakama hiyo kutokana
na shauri lililofunguliwa na mtumishi huyo.
Kesi hiyo yenye namba CMA/TRM/07/2013 itasikilizwa Aprili 8, mwaka huu.
Katika kesi hiyo mwalimu huyo anaitaka halmashauri hiyo imrejeshe
kazini bila masharti. Mwalimu huyo aliondolewa kazini Machi 31, mwaka
2012 bila kupatiwa barua ya kumwachisha kazi.
Alidai alipatiwa barua ya kusimamishwa kazi tangu Desemba 30, mwaka
2010 na kutakiwa kulipwa nusu mshahara, lakini tangu wakati huo amekuwa
hapokei mshahara wowote.
Mfanyakazi huyo alisimamishwa kazi kwa madai ya utoro kazini na suala lake linashughulikiwa na TSD.
TSD hadi sasa haijatoa uamuzi wa mwalimu huyo kuondolewa kwenye ajira
yake ambayo ipo chini ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
No comments:
Post a Comment