
HAKUNA njia ya mkato ya kufanikiwa katika biashara. Kama ipo,
mambo yangekuwa ni rahisi, na tusingesikia habari zinazoelezea biashara
zimekufa, ama kukosa mwelekeo. Lakini ukiangalia biashara zenye
mafanikio, utaona mambo fulani fulani yanafanana katika uendeshaji wake.
Kuna hatua ambazo kampuni hizo zinafuata. Njia hizo ndizo
zinazowafikisha kwenye mafanikio hayo. Zifuatazo ni baadhi ya njia
ambazo wajasiriamali wanazitumia na zimewafanya wafanikiwe katika
biashara zao.
Ni vema ukafahamu kuwa kila unayekutana naye mtaani ana wazo la
biashara. Lakini wazo moja kati ya mia uliyoyapata litakufanya uwe
mjasiriamali. Lakini watu wengi wanaogopa kufanya biashara ambayo
itawapatia hasara, au itawafanya watumie mshahara wao kwa ajili ya
kuiimarisha. Kufanikiwa katika biashara, inakubidi ufanye uamuzi
thabiti. Inakubidi kuwa jasiri wa kutumia wazo lako.
Pili, ndoto yako ndiyo itakayokufanya kuwa mfanyabiashara aliyefanikiwa katika kiwanda cha burudani.
Lakini huwezi kuwa na biashara hiyo kama haujui kitu chochote kuhusu filamu pamoja na ujuzi wa hali ya juu wa teknolojia.
Inakubidi kwanza kuwa na uelewa kuhusu kile unachotamani kukianzisha ili uweze kukisimamia.
Mjasiriamali yeyote anajifunza kutokana na makosa. Hapa namaanisha
kuwa, kila hatua anayoifanya ambayo inasababisha ashindwe katika
biashara yake, inabidi afanye utafiti na kujua ni jinsi gani atahimili
changamoto hiyo, na kujitahidi asirudie kosa lililotokea katika biashara
husika.
Hatakiwi kukata tamaa, pia anatakiwa kuwa na mawazo chanya kila wakati katika maisha na ujasiriamali anaoufanya.
Mwanzo wa biashara yako utaweza kufanya makosa mengi. Chukua makosa
hayo kama ndio kipimo chako cha kufanikiwa, jitahidi kutorudia.
Kila changamoto unayokutana nayo ifanye kuwa ndiyo nafasi ya kujifunza na kufanya vizuri zaidi katika biashara yako.
Wakati unamiliki biashara unakuwa na uhuru. Tumia uhuru huo kufanya
vizuri zaidi, pia jifunze kuwa na nidhamu ya biashara. Hapa itakubidi
ufanye kazi kwa bidii na kujituma zaidi.
Inabidi ujikite zaidi kwa wazo lako la biashara na wale wote ambao
walikuwa sehemu ya kukamilisha ndoto yako, ambao wanaweza kuwa
wafanyakazi wako, marafiki ama familia yako.
Kama utakuwa umejizatiti katika biashara yako ndipo utakapofanya
jitihada zaidi za kuiboresha ambazo zitakuwezesha kufanikiwa sana.
Kumbuka kuwa hakuna mti uliozaa matunda kwa usiku mmoja. Pale mti unapochomoza, ili ukue unapitia hatua mbalimbali.
Kama mjasiriamali inakubidi uwe na roho ya uvumilivu ili matunda ya
kazi yako yaweze kukomaa. Pia kuongeza jitihada zaidi katika kila hatua,
kuwa imara na mwenye malengo.
Kuwa tayari kukubali makosa na kuyasahihisha. Kuwa imara pia ni ufunguo wa mafanikio katika biashara.
Pia mawazo mgando hayahitajiki katika biashara. Inakupasa kujifunza na
kuiga mambo mazuri kutoka kwa wengine, pia ukumbuke kuwa kila siku ina
jambo jipya la kujifunza kuhusu biashara.
Mawazo yako yatawafikia wateja wako kwa urahisi, japo katika hatua za
awali za biashara zako inawezekana ukapata wateja wachache. Hivyo
inakubidi kuonesha bidhaa zako kwa wateja wako.
Kuwa tayari kujibu maswali kutoka kwa wateja wako, kwa mfano: “Bidhaa
zako zina kitu gani cha tofauti zaidi ya wafanyabiashara wengine?”
Kama utakuwa na majibu ya kuwaridhisha utakuwa umefanikiwa katika hilo.
Pia ukumbuke kuwa kila biashara ina ‘risk’. Hivyo uwe tayari
kukabiliana nazo. Ni vema ukawashirikisha wataalamu katika biashara
yako.
Hizi ni baadhi tu ya hatua ambazo zitakusaidia katika kuboresha ama kukabiliana na changamoto katika biashara yako.
Maisha Yetu na Lucy Ngowi
No comments:
Post a Comment