TAARIFA KWA UMMA
 
 
Ndugu wanahabari na wakazi wote wa mkoa wa Arusha.
Kwanza kabisa, tunapenda kutoa pole za dhati kwa familia, ndugu jamaa, wanachuo na jumuia yote ya chuo cha uhasibu Arusha wa marehemu Henry Kago aliyefariki juzi usiku kwenye tukio la kutisha na kuhuzunisha sana.
Tumesikitishwa na msiba huu na tunawaombea wote Mungu awapatie faraja na utulivu katika kipindi hiki kigumu.
Katika tukio hili, mbunge wa 
Arusha Mjini 
Mhe Godbless Lema alijulishwa na kama kiongozi alifika ili 
kuona namna atakavyoweza kutoa msaada hasa baada ya wanachuo kuonyesha 
hisia zao kwa vile hawakuona kupata msaada kutoka kwa uongozi wa chuo na
 serikali kwa ujumla. Hili ni tukio la pili la mauaji ya mwanachuo 
sambamba na matukio mengi ya wanachuo kuvamiwa na kunyang’anywa mali 
zao.
Mhe Lema aliwatuliza wanachuo na kuchukua hatua za kumjulisha mkuu wa Mkoa Mhe Mulongo aje na kuzungumza na vijana hawa.
Hata hivyo ujio wa mhe Mulongo 
ulionekana haukuwa na dhamira ya dhati na badala yake alionyesha 
madharau makubwa ambayo mpaka sasa nashindwa kuelewa alikuwa na maana 
gani kuonyesha tabia ya kipuuzi namna ile kwa vijana waliokuwa wamepata 
msiba wa mwenzao.
Picha za video zinaonyesha kwa dhahiri jitihada kubwa aliyoifanya mhe Lema kuwatuliza vijana hawa na kuwaomba wawe wavumilivu.
Baada ya tukio zima kukumbwa na 
vurugu ambazo kimsingi chanzo ni tabia aliyoinyesha Mhe mulongo kwa 
vijana hawa, mkuu wa mkoa aliongea na waandishi wa habari kuwa chanzo 
cha vurugu hizo ni Mhe Lema na kuwa tukio zima la mauaji haya ni masuala
 ya kisiasa na kuwa wanasiasa wamepanga mambo haya ili kujipatia 
umaarufu, hii na kauli ya mwendawazimu kabisa. Katika hatua hii 
walimkamata Wakili Mhe Albert Msando ambaye pia ni diwani wa CHADEMA na 
kumchukua kwa mahojiano. 
Kwa ujumla msingi wa suala la kumtafuta muuaji wa Henry umepabadilika na kuwa kumtafuta Lema. 
Tunataka tuweke kumbukumbu hii 
kwa wakazi wa Arusha, jambo hili ni mfululizo wa matukio mengi 
yasiyoonyesha weledi ya Mhe mulongo ambayo amekuwa akifanya na kama 
chama tunamtakia hivi kikombe kitakopajaa atatambua maana ya nguvu ya 
umma. Anaweza kudharau maneno haya, afanye hivyo kwa vile anajisikia 
kuwa yupo na mamlaka ya kiserikali lakini tunarudia kusema kuwa kamwe 
hatuwezi kuendelea kuvumilia uongo na akili mbovu za namna hii kuongoza 
watu wenye akili. Narudia kusema hatutavumilia uongo wa namna hii 
kuendelea kusemwa halafu familia iliyopoteza mtoto wao mpendwa ikiwa 
katika masononeko makubwa.
Sasa mhe Mulongo na watu wake 
wajiandae vema maana tumejiandaa kupambana na watu na/au viongozi ambao 
tumeshajua ni wapotoshaji na wahuni na wanafanya mambo ya kihuni. 
Tunawaomba wakazi wa Arusha 
wawakatae viongozi wapotoshaji na wahuni, wasiwape ushirikiano wowote 
ule na sisi tutasimama na wananchi kwa pamoja katika mazingira yote ili 
kudumisha uongozi bora wenye kujali na kuheshimu raia wote kwa 
mustakabali wa mkoa wetu kiuchumi na katika kujenga utulivu.
Imetolewa leo tarehe 25 Aprili 2013
Amani Golugwa
KATIBU WA CHADEMA – KANDA YA KASKAZINI.
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment