WAKILI
wa Serikali, Prudence Rweyongeza amedai mahakamani kwamba, Mkurugenzi
wa Mashitaka nchini (DPP) alikuwa sahihi alipotoa hati ya kufuta
mashitaka ya ugaidi dhidi ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA,
Wilfred Lwakatare na kuyarudisha upya.
Pia alidai DPP alikuwa sahihi kuwashtaki kwa makosa hayo na ni mapema sana upande wa utetezi kuhoji uhalali wa mashtaka hayo kwa sababu upelelezi haujakamilika.
Hayo yalidaiwa jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Wakili Rweyongeza mbele ya Jaji Lawrence Kaduri, wakati maombi ya kupinga utaratibu wa DPP kumfutia mashtaka Lwakatare na Ludovick Joseph, kisha kuwakamata na kuwafungulia tena mashtaka mengine.
Kabla ya kuanza kusikiliza maombi hayo, wafuasi wa CHADEMA na wengine waliovutiwa na kesi hiyo, walifurika katika lango la kuingia mahakama ya wazi kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo bila mafanikio.
Mahakama ilifurika watu katika korido zote huku askari wakiwa wamelinda mlango wa kupandisha katika chumba hicho kidogo, wakizuia watu ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari.
Walioruhusiwa kuingia humo ni washtakiwa wote wawili, mawakili wao na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Katibu wake, Dk. Willibrod Slaa.
Akiwasilisha hoja Rweyongeza alidai DDP alitumia madaraka yake vizuri kulinda haki kama Katiba inavyosema na kwamba alikuwa na sababu za kufuta mashtaka na kuwafungulia upya washitakiwa.
Alidai maombi ya Lwakatare hayana msingi kwa sababu kuruhusu kesi namba 37 iendelee kusikilizwa ni sawa na kuruhusu makosa yaendelee kufanyika na hoja ya kuhoji uhalali wa mashtaka iliwasilishwa wakati si muafaka.
“Kesi bado iko katika uchunguzi, mashtaka yanaweza kubadilika wakati wowote au kufutwa na washtakiwa kuachiwa, kwa wakati huu mashtaka hayana upungufu,”alidai Rweyongeza.
Mawakili wa Lwakatare, Tundu Lissu, Peter Kibatala, Profesa Abdallah Safari na Nyaronyo Kicheere waliwasilisha mahakamani pingamizi wakiiomba mahakama ifanye marejeo ya mwenendo wa kesi katika Mahakama ya Kisutu.
Kwa mujibu wa maombi hayo ya marejeo namba 14 ya mwaka 2013, lengo la kuiomba mahakama hiyo iitishe majalada hayo, ni kufanya uchunguzi ili kujiridhisha yenyewe kuhusu usahihi na uhalali wa mwenendo wake.
Pia mawakili hao waliiomba Mahakama Kuu ifanye marejeo au kutengua hati ya DPP ya kuwafutia mashtaka watoa maombi, kabla ya kuwakamata na kuwafungulia tena mashtaka hayo hayo.
No comments:
Post a Comment