KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kwa
mara nyingine imezidi kumbana Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Abdulrahman Kinana ikimtaka mwendesha mashitaka wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki kumfungulia mashitaka ya kutorosha pembe za ndovu katika
mahakama ya Afrika Mashariki.
Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo jana kwa Wizara ya Ushirikiano wa
Afrika Mashariki kwa mwaka 2013/2014, Raya Ibrahim Khamis kwa niaba ya
msemaji mkuu Ezekiel Wenje, alitaka Tanzania iombe msaada wa Kenya
yenye ubalozi wa Vietnam ili kurahisisha upatikanaji wa ushahidi badala
ya kutegemea ubalozi wake ulioko China.
Raya alisema madhumuni ya kumfungulia kesi Kinana yana lengo la
kuudhibiti mtandao wa majangili na wafanyabiashara haramu ya pembe za
ndovu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Alibainisha kuwa wanataka Kinana afunguliwe kesi kutokana na meli
anazosimamia mojawapo ilikamatwa na shehena za pembe za ndovu huko
Vietnam mwaka 2009.
Hii ni mara ya pili kwa kambi hiyo kuibua tuhuma hizo dhidi ya Kinana
ambapo kwa mara ya kwanza msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara
ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa alihoji jambo hilo na
kupata upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa CCM.
Raya alisema kuwa biashara haramu ya pembe za ndovu katika ukanda wa
Afrika Mashariki inakua kwa kasi jambo linalotishia kutoweka kwa
wanyama ndovu ambao ni kivutio kikubwa cha utalii.
Alisema kuwa taarifa katika mtandao wa habari wa “Annamiticus”
(www.annamiticus.com) zinasema kwamba mwaka jana, makontena mawili
kutoka Kenya na Tanzania yalikamatwa huko Hong Kong yakiwa yamebeba
tani 4 (kilo 4,000) za pembe za ndovu.
“Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kontena lililotoka Tanzania lilikuwa
limeandikwa “plastic scrap” ikimaanisha kuwa lilikuwa na vifaa ya
plastiki, lakini baada ya kufunguliwa kulikuwa na vipande 972 vya pembe
halisi za ndovu zenye uzito wa kilogramu 1,927 pamoja na kilo moja na
nusu ya unga wa pembe za ndovu zilizosagwa.
“Kontena lililotoka Kenya lilikuwa limeandikwa “roscoco beans” yaani
maharage aina ya roscoco, lakini lilipofunguliwa kulikuwa na vipande
237 vya pembe za ndovu sawa na kilogramu 1,884,” alisema.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa taarifa hiyo, wingi wa pembe hizo za
ndovu zilizokamatwa, unadhihirisha kwamba tembo 600 kwa uchache
waliuawa.
Aliongeza kuwa mwezi uliopita kontena jingine limekamatwa limesheheni
pembe za ndovu 113 huko China zenye thamani ya dola za Marekani
400,000 likiwa limeandikwa kwamba limebeba vipuri (spareparts) kutoka
Burundi.
“Kwa kuwa Burundi haina bandari, kuna uwezekano mkubwa kwamba kontena
hilo lilipitia bandari ya Tanzania, na hivyo kuna uwezekano pia kwamba
pembe hizo zinatokana na tembo waliouawa Tanzania,” aliongeza.
Alisema kambi hiyo inataka kujua kama Serikali ya Tanzania imefanya
mawasiliano na Burundi ili kujua ukweli kuhusu kontena lililosheheni
pembe za ndovu lililokamatwa huko China.
Aliongeza kuwa kwa kuzingatia utekelezaji wa mpango mkakati wa amani
na usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kubadilishana taarifa za
uhalifu na usalama, ni vema serikali ikiwasiliana na wote wanaoweza
kukamilisha uchunguzi husika.
Alisema kuwa kuna Watanzania walioshutumiwa na kusutwa kuhusika na
mtandao huu wa biashara hii haramu ya pembe za ndovu akiwemo Katibu
Mkuu wa CCM, Kinana.
“Kwa kuwa Serikali ya Tanzania inaonekana dhahiri kumtetea na
kumlinda mtu huyu kwa kuwa ni kiongozi mkubwa wa chama tawala, kama
alivyofanya Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi alipokuwa anatoa
mchango wake kwenye bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Aprili 30
mwaka huu.
“Na kwa kuwa tembo wengi wa Afrika Mashariki wanazidi kupotea kila
siku kutokana na biashara hii haramu ya pembe za ndovu, jambo ambalo
linaikosesha Jumuiya ya Afrika Mashariki mapato yatokanayo na utalii na
hivyo kuiweka hatarini sekta ya utalii ya Afrika Mashariki, watu hawa
lazima washtakiwe,” alisema.
Raya pia aligusia uhuru wa habari kwa nchi wanachama huku akinukuu
taarifa ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ya Mei 20 mwaka huu
ambayo ilisema kuwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameamuru kufungiwa
kwa gazeti la kila siku la nchi hiyo la “The Daily Monitor”, na gazeti
lingine la “Red Pepper”.
Hatua hiyo ni kutokana na kuchapisha habari iliyofichua njama za Rais
Museveni za kumuandaa mtoto wake, Muhoozi Kainerugaba ambaye ni
brigedia wa jeshi kuwa rais wa nchi hiyo baada ya yeye kuondoka
madarakani.
Hata hivyo, baada ya kuhitimisha hotuba yake, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliomba
mwongozo wa kiti akitaka wapinzani wakemewe kwa kukiuka kanuni na
kutaja majina ya viongozi wakuu wa nchi kwa dhihaka.
“Mimi sitaki kuzungumzia suala la Kinana maana hizo ni porojo wacha
waendelee, lakini nazungumzia ukiukwaji wa makusudi wa kanuni na
kumtaja Rais Museveni kwa mambo ambayo eti msemaji ameyasikia kwenye
redio pamoja na lile la Kinana japo tumeishajibu, lakini wanaendelea
kujifurahisha. Naomba ukemee jambo hili,” alisema.
Hata hivyo, baada ya Lukuvi kuketi, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
naye aliomba mwongozo akitumia kanuni inayomruhusu mbunge kunukuu
taarifa kwenye vyombo vya habari akisema kuwa Raya alikuwa sahihi.
Sitta amkingia kifua
Akijibu hoja hiyo wakati wa majumuisho, Waziri wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta aliwataka CHADEMA wamuache Kinana afanye siasa na majibu
watayaona mwaka 2015.
Sitta alisema CHADEMA imekuwa ikitumia nguvu kulazimisha hoja zao na
inaonekana Kinana ndiye anayewakera kwa kuwa hatoki midomoni mwao.
“Kila siku Kinana…Kinana…jamani hebu acheni kumhusisha na biashara haramu ya pembe za ndovu,” alisema.
Chanzo ni Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment