JUMUIYA ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK) wamewataka Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda na Waziri wa Uchukuzi, Dk.
Harrison Mwakyembe kuwasaidia kutatua tatizo la kodi na ucheleweshwaji
wa mizigo unaofanywa na mawakala.
Akizungumza katika kikao cha dharura kilichofanyika jijini Dar es
Salaam jana, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Mathias Makoyi, alisema tatizo
la kuzuiwa kwa makontena yao na ushuru wa forodha kuwa mkubwa
vimewafanya wafanyabiashara wengi kushindwa kulipa marejesho waliyokopa
benki.
Makoyi alisema tatizo hilo limewakumba kwa kipindi cha miezi miwili
sasa, na kwamba limesababisha umauti kwa wafanyabiashara walioshindwa
kutoa mizigo yao na kufilisiwa na benki.
Katibu wa chama hicho, Sued Hamisi, alisema tatizo lililopo ni kati
ya mawakala na waagizaji wa mzigo kutokana na baadhi ya mawakala
kukwepesha kodi, hali iliyosababisha wafanyabiashara wa nchi jirani
kukimbia.
“Tulitaka kuandamana na kufunga maduka yote lakini tukaona njia
sahihi ni mazungumzo, hivyo tunawaomba viongozi wetu watusaidie hili
tatizo liishe maana tunafilisika na mikopo inatudai,” alisema.
No comments:
Post a Comment