MKUU wa Wilaya ya Iramba, Yahaya Nawanda, amewahimiza wanaume
kuwasindikiza wake zao wanapokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za
mama na mtoto ili nao wakasikilize ushauri nasaha ili iwe rahisi kwao
kutekeleza.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa changamoto hiyo kwenye hafla fupi ya
kuzindua huduma ya kliniki tembezi iliyofanyika kwenye kituo cha afya
cha Ndago, wilayani hapa.
Alisema halitakuwa jambo la busara kwa wanaume wanapowaona wake zao
wakienda kliniki na wao wakabaki nyumbani ama kwenda kwenye shughuli
nyingine.
“Naomba niwaase wanaume twende kliniki na wake zetu, haitakuwa na
maana yeyote ile iwapo mwanamume atamuacha mkewe anakwenda kliniki peke
yake,” alisema.
Kwa mujibu wa Nawanda, mwanamume anapokwenda na mkewe kliniki hupatiwa
ushauri nasaha na wataalamu wa afya juu ya elimu ya kulea mimba pamoja
na kutunza mtoto na kuongeza kwamba hata mtoto akizaliwa anakuwa na
uhakika wa kuishi.
Mwenyekiti wa wakuu wa wilaya wa Mkoa wa Singida, Mwalimu Queen Mlozi,
alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha watendaji pamoja na wananchi wa
wilaya hiyo kutobweteka kutokana na sifa walizopata za kuongoza katika
kutoa huduma za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Fatma Toufiq, alisema ushindi wa wilaya
hiyo katika sekta ya afya, usibakie kwenye wilaya moja ya mkoa huo na
badala yake wilaya zote ziwe mabingwa wa kutoa elimu hiyo kwa wilaya
nyingine hapa nchini.
No comments:
Post a Comment