JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewakamata
watuhumiwa wa ujambazi watano wanaodaiwa kupora sh milioni 46 za
mfanyabiashara wa bia wilayani Temeke, Ivon Urio.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda
wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema tukio hilo lilitokea
juzi saa tano asubuhi na watuhumiwa wote wamekiri kuhusika na tukio
hilo, na kumtaja mwenzao John Tesha kwamba ndiye aliyekimbia na fedha
hizo.
Kova aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Bernards Mashamba, Steven
Thadeo, Adams Isudor, Johns Benja na Sultanis Kipensa huku juhudi za
kumtafuta mwenzao aliyekimbia zikiendelea.
Alisema pesa hizo zilikuwa zimewekwa katika boksi kwa ajili ya
kupelekwa benki ya BOA ghafla mfanyabiashara huyo akavamiwa na
watuhumiwa hao waliokuwa na bunduki kubwa moja na bastola mbili
wakitumia pikipiki mbili aina ya Boxer mojawapo ikiwa na namba za
usajili T 311 CGE rangi nyekundu.
Kova alitaja maeneo waliyokamatiwa majambazi hao ni Chamanzi, Manzese, Keko, Kongowe Kizinga na Mtoni Mtongani.
Katika hatua nyingine, Kova alisema pikipiki 300 zimekamatwa kati ya
hizo 201 ni aina ya Boxer ambazo zinasadikiwa kuwa kwa kiasi kikubwa
zinatumiwa na majambazi.
Aliongeza kuwa wanaandaa utaratibu wa kuzipaka rangi pikipiki zote
kama zilivyo teksi ili zijulikane wilaya zinakotoka na wamiliki wake.
Kamanda Kova alisema mpango huo utasaidia kudhibiti uhalifu na ajali zinazotokea mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment