HATIMAYE kitita cha dola 70,000 za Marekani (zaidi sh Mil. 100)
kimemaliza ‘ngonjera’ za usajili wa kiungo wa kimataifa ya Yanga,
Haruna Niyonzima, raia wa Rwanda.
Niyonzima ambaye mkataba wake wa kukipiga kwa mabingwa hao wa soka
Tanzania Bara ulikuwa umemalizika msimu huu, alitawala vichwa vya
mashabiki wengi wa soka hapa nchini, baada ya kudaiwa kugoma kuongeza
mkataba na kutaka kutimkia kwa mahasimu wao Simba.
Niyonzima, nyota aliyeziteka hisia za mashabiki wa klabu hiyo,
ameamua kubaki kuendelea kuitumikia klabu hiyo kwa miaka miwili, baada
ya uongozi kuridhia kumpa kitita hicho.
Mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga, ambaye hakutaka jina lake kutajwa
gazetini, alisema wamejitahidi kupigana kufa au kupona ili mchezaji
huyo aendelee kuitumikia klabu hiyo na kuepusha madaraka yao kuingia
doa.
“Uongozi tumepigana sana huku na kule ili kuhakikisha Niyonzima
anaendelea kucheza Yanga na ndiyo maana tumefanikisha mara baada ya
kumpa dola 70,000 ili aweze kumwaga wino na tunamshukuru Mungu
tumefanikiwa,” alisema kiongozi huyo.
Aidha, chanzo hicho kilisema kuwa kwa sasa uongozi umepumua mara
baada ya kumaliza suala la Niyonzima, ambalo lilionekana kuwa gumzo na
kuwanyima usingizi mashabiki, wadau na wanachama wa Yanga.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako
aliyeambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Abdallah Binkleb,
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Musa Katabaro na Mjumbe wa Bodi ya
Wadhamini, Fransis Kifukwe alisema wameamua kuutangaza mkataba mpya wa
mchezaji huyo, kutokana na simu mbalimbali walizokuwa wanazipata kutoka
kwa mashabiki wao wenye mapenzi ya dhati na klabu hiyo.
Mara baada ya kumtambulisha upya Niyonzima, Mwalusako alimpa zawadi
ya kofia na skafu zenye nembo na jina la klabu hiyo ikiwa ni sehemu ya
kuthamini mchango wake Jangwani.
Akizungumzia mkataba huo, Niyonzima alisema yeye anaheshimu mpira kwa
kuwa ndiyo kazi yake na kuwa uvumi uliokuwa umetapakaa kuwa anakwenda
Simba, yeye ndiye mwamuzi wa kila kitu na kudai kuwa sio kusema kuwa
uwepo wake Yanga unamnyima nafasi ya kuongea na watu wengine.
“Mimi kumaliza mkataba Yanga sio kwamba utanizuia kuongea na timu au
mtu yeyote, hayo ni maamuzi yangu mwenyewe ila nimesaini Yanga miaka
miwili,” alisema Niyonzima.
Naye Binkleb alisema mbali na Niyonzima, kuna nyota watatu pamoja na
Kocha Mkuu wao Ernie Brandts, hawana mikataba hadi sasa baada ya awali
kuwa imemalizika.
Aliwataja nyota hao kuwa ni Nizar Khalfan, Hamis Kiiza na Nurdin
Bakari na kudai kuwa wako katika mazungumzo nao ili kuwapa mikataba
mingine, huku kwa upande wa Brandts, wanamsubiri atakaporejea Juni 2
akitokea nchini Uholanzi katika mapumziko.
No comments:
Post a Comment