KOCHA mkuu wa klabu ya Yanga, Ernie Brandts, anatarajiwa kurejea nchini Rwanda kuinoa timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’.
Brandts kabla ya kujiunga na Yanga na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa
Ligi kuu ya Vodacom msimu huu, alitokea Rwanda alikokuwa akiinoa klabu
ya APR.
Rafiki wa karibu wa kocha huyo ambaye hakutaka kutajwa hadharani,
aliipasha Tanzania Daima jana kuwa Brandts ameitwa nchini Rwanda kwa
ajili ya kukinoa kikosi hicho kilichokuwa kinanolewa na Milutin
Sredojevic ‘Micho’ ambaye alitupiwa virago hivi karibuni kutokana na
timu hiyo kuvuna matokeo mabovu katika mechi zake kadhaa. Micho hivi
sasa kaula timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’.
Rafiki huyo alisema Brandts alimwambia kuwa anakwenda kufanya nao
mazungumzo kwa kuwa tayari ameishapata ofa hiyo na kudai kuwa itakuwa
ngumu kurejea Yanga kama mambo ‘yatatiki’ nchini Rwanda.
“Brandts kurudi Yanga ni mpaka mambo yakikataa Rwanda, ila ni asilimia
ndogo sana ya kurudi Yanga, kama ambavyo aliniambia mimi,” alisema
rafiki huyo.
Shirikisho la soka nchini Rwanda, Ferwafa, lilimtupia virago Micho,
April 17, mwaka huu, katika taarifa iliyotumwa na Katibu Mkuu wa
Ferwafa, Michel Gasingwa, kupitia mtandao, ambayo ilidai kuwa kamati ya
utendaji ilifikia uamuzi huo ili kuinusuru timu isiendelee kuboronga
katika mechi zake.
No comments:
Post a Comment