WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amehimiza vijana nchini kuwa na
uthubutu wa kujaribu kuzifanyia kazi fursa zilizopo katika sekta
mbalimbali kwenye maeneo wanayoishi.
Pinda alitoa kauli hiyo mjini hapa jana alipozungumza na mamia ya
vijana wa mji wa Dodoma na Dar es Salaam baada ya kupokea maandamano ya
kutangaza kampeni ya kupenda na kutumia bidhaa na huduma za Tanzania
maarufu kama “Made In Tanzania” yaliyofanyika kwenye Viwanja vya
Mwalimu Nyerere.
Alisema kwa mujibu wa Sensa ya Makazi na Watu ya mwaka 2012,
Tanzania ina idadi kubwa ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi,
wanaofikia asilimia 52 ya watu wote, na wengi wao ni vijana na asilimia
48 ni wazee na watoto.
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda.
“Hivyo basi, nchi yetu inaweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kama
kundi hili lote la vijana litaamua kutumia kikamilifu fursa zilizopo
nchini za kujiletea maendeleo,” alisisitiza.
Alisema wako watu walianza ujasiriamali kwa kuuza karanga, lakini
walipanda hadi kuwa na biashara kubwa kwa sababu walitambua fursa
zilizokuwepo na wakazifanyia kazi.
“Kikubwa ni kuwa na dhamira na malengo, lakini fursa ziko kwenye
kilimo, viwanda, ufugaji nyuki, ufugaji kuku wa asili ama mapishi ya
chakula,” aliongeza.
Alisema anafurahishwa na mwamko uliopo hivi sasa kwa baadhi ya vijana
waliohitimu vyuo vikuu ambao wameamua kujiunga kwenye vikundi na
kuanzisha miradi yao.
“Wako vijana waliohitimu ambao wameomba misaada serikalini na
wakaanzisha miradi huko waliko. Wengine wako Igunga, Iramba, Tarime,
Rufiji na Mkuranga,” alifafanua.
Alisema wako walioamua kujihusisha na kilimo cha alizeti na wengine
wameamua kufuga kuku wa asili na kuwauza Dar es Salaam ambako walibaini
kuna soko la uhakika kwa bei ya sh 10,000 hadi sh 15,000 kwa kuku
mmoja.
Alisema licha ya kudumisha mapenzi ya dhati na kujenga uzalendo kwa
nchi na watu wake, kampeni hiyo pia inalenga kuonyesha ufahari wa yote
yanayowazunguka Watanzania, ufahari ambao upo ndani ya kila mmoja.
Kampeni hiyo ya Made in Tanzania inayoendeshwa na kampuni ya Clouds
Media Group ilianza Machi, mwaka huu, kwa lengo la kutambua watu,
bidhaa, mashirika, muziki na utamaduni wa Kitanzania na imelenga
kutangaza bidhaa na huduma za Tanzania.
No comments:
Post a Comment