SERIKALI barani Afrika zimetakiwa kutoa msaada kwa wakulima
wanawake kama bara hilo linataka kufikia maendeleo endelevu kijamii na
kiuchumi.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Kilimo na
Maendeleo Vijijini wa Nigeria, Dk. Akinwumi Adesina, katika kongamano la
kikanda la kilimo la Muungano wa Umoja wa Vyama vya Kilimo Kusini mwa
Afrika (SACAU) na kuongeza kuwa ni muhimu serikali na wadau wengine
wanaosaidia maendeleo ya kilimo wakajua kuwa wakulima wengi katika bara
hilo ni wanawake.
Kongamano hilo litakaloangalia kwa undani suala la jinsi ya kuhudumia
kifedha kilimo cha Afrika linatayarishwa na Baraza la Kilimo na Mifugo
Tanzania (ACT) kwa kushirikiana na SACAU.
“Wakulima wanawake wanahitaji kupata mikopo nafuu, uhakika wa ardhi,
na teknolojia,” alisema na kuongeza kuwa mustakabali wa sekta ya kilimo
katika bara la Afrika sio wa uhakika kama wanawake wakulima watawekwa
pembezoni na mipango ya maendeleo inayohusu sekta hiyo.
Kongamano hilo linaloangalia kwa undani swala la jinsi ya kuhudumia
kifedha kilimo cha
Afrika linatayarishwa na Baraza la Kilimo na Mifugo
Tanzania (ACT) kwa kushirikiana na SACAU.
Waziri huyo alisema hakuna sababu ya bara la Afrika kuagiza chakula
toka nje wakati zaidi ya asilimia 60 ya ardhi inayofaa kwa kilimo na
ambayo bado haijatumika iko katika bara hilo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa SACAU, Ishmael Sunga, alisema wakulima wa
Afrika hawawezi kuendelea kwa haraka na kuwa wakubwa kama hawataweza
kupata huduma za uhakika za kifedha.
Mkurugenzi wa maendeleo ya mazao toka Wizara ya Kilimo, Usalama wa
Chakula na Ushirika, Dk. Mshindo Msolla, alisema ni muhimu kwa serikali
za Afrika zikajitahidi kuwa na usalama wa chakula katika kila nchi kabla
ya kufanya lolote.
Akizungumza kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo, Dk. Msolla alisema
serikali ya Tanzania inafanya juhudi kubwa kufikia mapinduzi ya kilimo
kupitia mipango mbalimbali kama Kilimo Kwanza na mpango maalumu wa
kuendeleza kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
No comments:
Post a Comment