VIJIJI 91 katika jimbo la Bukoba Vijijini vinakabiliwa na
ukosefu wa majisafi na salama jambo ambalo linasababisha uzalishaji
kushuka.
Hayo yalielezwa bungeni jana na mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson
Rweikiza (CCM), alipouliza swali la nyongeza kwa kutaka serikali ieleze
ni lini itapeleka maji katika vijiji hivyo.
“Jimbo la Bukoba Vijijini lina vijiji 92; ni kijiji kimoja tu ambacho
kina maji, nataka kuelezwa ni lini wananchi wa vijiji 91 wataweza
kupatiwa maji ambao waliamua kujitolea kuchanga fedha kwa ajili ya
kununua mashine ya kuchimba visima?” alihoji Rweikiza.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kuelewa ni kwa nini vijiji
vya Kibona Ibwera, Rukindo Kitahya na Katale havikupewa kipaumbele
katika kutekeleza mradi wa maji kutokana na ukubwa wa tatizo hilo katika
wilaya ya Bukoba Vijijini.
Aidha, alitaka kuelezwa ni lini serikali itatekeleza miradi hiyo, ili kuwaondolea kero ya kukosa majisafi na salama.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Kassim Majaliwa, alisema halmashauri
ya wilaya ya Bukoba Vijiji imekamilisha usanifu wa miradi katika vijiji
10 walivyochagua kama vipaumbele vyao.
Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Kibirizi, Itongo, Lukindo, Katale, Mashule, Kitahya, Ibwera na Kyamulaile.
“Ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mashule umekamilika Machi
mwaka huu na wananchi wanapata huduma ya maji, halmashauri inakamilisha
taratibu za kusaini mkataba wa mkandarasi wa ujenzi wa mradi katika
kijiji cha Kyamulaile na taratibu za manunuzi kwa ajili ya kuwapata
makandarasi wa ujenzi kwa ajili ya vijiji viwili vya Kibana na Kitahya
zinaendelea,” alisema.
Aidha alisema ujenzi wa mradi wa Bituntu, Kibirizi, Itongo, Lukindo,
Katale na Ibwera utafanyika katika mwaka wa fedha wa 2013/14 ambapo sh
bilioni 1.3 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema katika mwaka 2001/13, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba
ilitengewa sh milioni 612.02 na hadi sasa sh milioni 416 zimeshatolewa
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.
No comments:
Post a Comment