KITUO cha Polisi Mwimbi, wilayani Kalambo, Rukwa, kimenusurika
kutekwa na kuchomwa moto baada ya kundi la wanafunzi wa Shule ya
Sekondari Mwimbi kuandamana kwa lengo la kukiteketeza kituo hicho.
Tukio hilo limetokea juzi, majira ya saa 8:30 usiku baada ya wanafunzi
hao kuiteketeza kwa moto nyumba ya mkuu wao wa shule na kisha kuelekea
kituo cha polisi kwa madai kuwa wanapinga kitendo cha polisi kuwadhibiti
kuiteketeza nyumba ya mkuu wa shule hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Rukwa, Moshi Chang’a, alisema chanzo cha
vurugu hizo ni wanafunzi kupinga adhabu ya kufyatua matofali kutokana
na kitendo cha kutoroka shuleni mara kwa mara.
Chang’a ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, alisema baada ya
wanafunzi hao kupewa adhabu hiyo waliandaa mkakati kwa siri na kisha
majira ya saa 6 usiku wakiongozwa na mwenzao, Aidan Lunguje, mwanafunzi
wa kidato cha nne walivamia nyumba ya mkuu wa shule, Willbrod Lucas na
kisha kuichoma moto.
Mwenyekiti huyo alisema kabla wanafunzi hao hawajaifikia nyumba hiyo,
mkuu huyo wa shule alitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi ukimtaka aondoke
nyumbani yeye na familia yake kwani kuna kundi la wanafunzi litavamia
muda si mrefu.
“Baada ya kupata ujumbe huo alimwamsha mkewe na watoto kisha kuingia
katika shamba la mahindi lililopo jirani na nyumba hiyo na ndipo muda
mfupi baadaye aliona kundi kubwa la wanafunzi wakiwa na mapanga, mawe,
visu, marungu na dumu la mafuta na kisha kuanza kuvunja milango ya
nyumba,” alisema.
Chang’a alisema baada ya wanafunzi hao kuvunja mlango na kukosa mtu
walianza kuiba mali mbalimbali kisha kuichoma moto nyumba hiyo na
kufyeka mazao yaliyokuwa shambani.
Wakati wanafunzi hao wakiendelea na uhalifu, polisi wa Kituo cha
Mwimbi walipata taarifa na kwenda eneo la tukio na ndipo wanafunzi
walipochukia na kuamua kwenda kuvamia kituo cha polisi ili wakichome
moto, lakini kabla hawajakifikia mwenyekiti wa kijiji alifyatua risasi
hewani, kitendo kilicholeta hofu na wanafunzi hao kutawanyika.
No comments:
Post a Comment